Morocco yapinga adhabu za Caf

Image caption Michuano ya shirikisho la kandanda barani Afrika, Caf iliyofanyika nchini Equatorial Guinea

Morocco imepinga vikwazo ilivyowekewa na Shirikisho la Kandanda barani Afrika, Caf kwa kushindwa kuandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2015.

Caf imeipiga marufuku Morocco kushiriki michuano miwili ijayo ya Caf, wakati huo huo ikikipiga faini chama cha mpira wa miguu cha nchi hiyo dola za Kimarekani milioni moja na kutaka fidia ya euro milioni nane, sawa na pauni za Uingereza milioni £5.9 kutokana na hasara iliyopatikana kwa nchi hiyo kushindwa kuandaa mashindano hayo.

Shirikisho la soka la Morocco, FRMF limesema "linapinga vikwazo vyote vya michezo na fedha".

Chama hicho kimesema kinaamini "hakuna msingi wa kisheria" kwa adhabu hizo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Issa hayatou rais wa Caf

Fainali za Afcon za mwaka 2015 zilizomalizika Jumapili, zilihamishiwa Equatorial Guinea baada ya Caf kukataa ombi la Morocco la kuahirisha fainali hizo kwa hofu ya ugonjwa wa Ebola, ambao uliyaathiri kwa kiasi kikubwa mataifa ya Afrika Magharibi ambako timu nyingi zilizofuzu kucheza fainali hizo zinatoka.

FMRF imesema katika mtandao wake: "kamati ya utendaji inasemekana kushtushwa sana na maamuzi yaliyochukuliwa na Caf.

"hayaendana kwa namna yoyote na hitimisho lililofikiwa katika mkutano wa kwanza na rais wa Caf, mjini Cairo, Misri."

Baada ya mkutano huo wa Januari na rais wa Caf, Issa Hayatou, rais wa shirikisho la mpira wa miguu la Morocco, Faouzi Lakjaa, amesema adhabu itakuwa tu ya fedha.

FRMF imesema kuwa"chukua hatua zote muhimu za kuunga mkono na maslahi ya mpira wa miguu wa Morocco".