JS Kabylie yashinda kesi dhidi ya Caf

Haki miliki ya picha
Image caption Mchezaji wa JS Kabylie, Mcameroon Albert Ebosse akipiga penalti wakati wa uhai wake dhidi ya USM Alger

Klabu ya Algeria ya JS Kabylie imeshinda rufaa yao dhidi ya adhabu ya kupigwa marufuku kwa miaka miwili kushiriki mashindano ya kandanda barani Afrika baada ya kifo cha mchezaji wao Albert Ebosse.

Ebosse raia wa Cameroon alipata majeraha makubwa ya kichwa kufuatia vurugu katika mechi za ligi ya Algeria mwezi Agosti,2014.

Mahakama ya kesi za michezo (Cas) "imeondoa adhabu hiyo mara moja" iliyokuwa imewekwa na Shirikisho la Kandanda barani Afrika, Caf mwezi Oktoba.

Cas imetoa hukumu kwa msingi kwamba Caf "haikuendana na sheria zake yenyewe" katika kutoa adhabu hiyo kwa kuifungia klaabu ya JS Kabylie.

"uamuzi wa kuifungia ulichukuliwa bila ya wawakilishi wa timu ya JSK kusikilizwa au hata kujulishwa juu ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya timu hiyo,'' imesema mahakama katika taarifa yake.

Awali ilifikiriwa kuwa Ebosse alifariki dunia baada ya kugongwa na kitu kilichorushwa na mashabiki baada ya timu yake kufungwa nyumbani 2-1 na USM Alger - ambapo alifunga goli.

Lakini uchunguzi ulionyesha kuwa Ebosse alifariki dunia yakiwa matokeo ya mapigo ya moyo kuliko ilivyodhaniwa kuwa alipigwa na kitu kilichorushwa.

Kabylie ilifuzu kucheza hatua ya mwanzo ya michezo ya klabu bingwa Afrika , baada ya kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Algeria.

Wamepangwa kuwa mwenyeji wa timu ya St. George ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa awali.