Uandikishaji daftari la wapiga kura bado

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Nembo ya Tume ya Uchaguzi Tanzania, chini yake ni mwanamke mmoja akimsaidia mwenzake kumwonyesha sehemu ya kupiga kura

Tume ya uchaguzi nchini Tanzania imesogeza mbele kwa wiki moja zaidi tarehe ya kuzinduliwa kwa zoezi la daftari la wapiga kura litakalotumia mfumo mpya wa kieletroniki yaani Biometric Voters Registration BVR. Zoezi hilo ambalo litaanza rasmi katika mkoa wa Njombe na baadae kufuatia katika mikoa mengine ya Tanzania hivi sasa linatarajiwa kuanza tarehe 23 ya mwezi huu badala ya tarehe 16 kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuvipa fursa vyama vya kisiasa kujiandaa na kuandaa watu wake. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa wamesema kauli hiyo haina ukweli wowote na kwamba tume inajikosha kwa sababu haina vifaa vya kutosha vya kuendesha uandikishaji huo. Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau kutoka Dar es Salaam ametuandalia taarifa ifuatayo:

Image caption Bunge la Tanzania

Wakati ikiwa imesalia miezi miwili tu na wiki kadhaa kabla ya tarehe iliyopangwa ya kupiga kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, wasi wasi unazidi kutanda miongoni mwa viongozi mbali mbali wa vyama vya kisiasa hapa nchini Tanzania, iwapo Tume ya Uchaguzi nchini humu itaweza kuboresha daftari la wapiga kura katika kipindi cha muda mfupi uliobakia. Baadhi ya viongozi hao wamesema kwamba licha ya tume hiyo kutovishirikisha vyama vya kisiasa katika baadhi ya maamuzi yake, lakini pia wamebaini kwamba mpaka sasa tume hiyo inakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya uandikishaji kwa sababu havijaingia nchini kama ambavyo anabaini Freeman Mbowe mwenyekiti wa Chadema.

Image caption Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF

Mfumo huyo mpya kwa Tanzania wa BVR utaigharimu tume kiasi cha fedha za kitanzania shilingi bilioni mia mbili na tisini na tatu ambazo mpaka sasa haijafahamika iwapo fedha hizo zimepatikana au la. Kwa upande wake, Prof. Ibrahim Lipumba ambae ni mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF anaelezea kuwa kukosekana kwa utaalam miongoni mwa wafanyakazi wa tume kunaweza kuwa kikwazo cha kufanikisha zoezi hilo.

Hata hivyo, Jaji Damian Lubuva ambaye ndiye mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania anasema madai hayo ni uoga wa wanasiasa ambao hawataki mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi.

Uandikishaji wapigakura umepangwa kufanyika nchi nzima kwa muda wa siku sitini kuanzia mkoani Njombe tarehe 23 mwezi huu ambapo watanzania zaidi ya milioni 23 wanatarajiwa kujitokeza katika uandikishaji huo. Hata hivyo kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, haijafahamika iwapo raia wengi watajitokeza kwa sababu kazi ya kuwahamasisha raia bado haijafanyika na vile vile baadhi ya watanzania wanaweza kuikosa fursa hiyo ikizingatiwa ni msimu wa wakulima kuingia mashambani kabla ya mvua za masika. Aboubakar Famau, Dira ya Dunia, BBC, Dar es Salaam.