Uchumi wa Ugiriki bado matatani Ulaya

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Alexis Tsipras waziri mkuu wa Ugiriki.

Hatua kali za kidiplomasia zinachukuliwa ili kuwepo kwa makubaliano yatakayosaidia kuipatia Ugiriki mikopo zaidi baada ya pendekezo hilo kukataliwa na Ujerumani.

Waziri mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, mazungumzo ambayo yametajwa kuwa na mwelekeo.

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni ile ya Ugiriki kuwaomba wakopeshaji wake kuipa mkopo wa miezi sita.

Gunter Krichbaum ni mwenyekiti wa kamati ya maswala ya ulaya katika bunge la Ujerumani na vile vile ni mjumbe wa chama cha Merkel cha CDU na kuzungumzia hali inavyokwenda."Tunajua fika kwamba Berlin ilikataa na hatuwezi kukubali kwa sababu kuna milango mingi iliyojificha, kama wasemavyo wenyewe Wajerumani. Serikali ya Ugiriki imeshauriwa vizuri tu, kutimiza ahadi yake, na sina maana ahadi ya serikali hii, bali ahadi za taifa zima. Sharti watimize ahadi zao bila hivyo sisi pia tutashindwa kutimiza ahadi zetu." amesema Bwana Krichbaum.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Angela Merkel Kansela wa Ujerumani

Wakati huo huo amefafanua kitu kinachohitajika kufuatia baada ya hapo. "Ugiriki hivi sasa sharti itimize kile ilichoahidi na kutekeleza mabadiliko na watakuwa wanafanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe. Kwa hiyo kile ninachoweza kutaraji ni kwamba hii serikali itauona ukweli huo. Tutaona kesho kwa sababu hivi sasa tuna baraza la mawaziri wa fedha. Wao ndio wataangalia iwapo suluhu itapatikana."

Ugiriki imejikuta katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi kutokana na kuzidiwa na deni la mabilioni ya fedha, huku ikisita kutekeleza masharti ya kupatiwa mikopo zaidi ili kunusuru uchumi wa taifa hilo la Ulaya.