Uandikishaji kwa Elektroniki umeshindwa?

Image caption Teknolojia mpya inaelezwa kukumbwa na changamoto inayokwamisha zoezi la uandikishaji kufanyika kwa ufanisi

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimeendelea kuishinikiza serikali kuachana na mpango wa kura ya maoni juu ya katiba inayopendekezwa na badala yake itatue changamoto zinazojitokeza wakati wa kuandika wapiga kura kwa kutumia mitambo ya BVR ili iweze kukamilika kwa ufanisi.

CHADEMA, CUF, NCCR MAGEUZI na NLD kupitia uongozi wao vimesema serikali inatakiwa kusikiliza malalamiko yanayotolewa juu ya namna mfumo wa uandikishaji unaoendelea ili kazi hiyo isikwamishe uchaguzi uchaguzi mkuu.

Moja ya changamoto zinazozungumziwa ni pamoja na idadi ndogo ya mashine hizo kuweza kumudu idadi ya wale wanaotakiwa kuandikishwa.

Awali, mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi alieleza BBC kuwa mpaka zoezi linaanza zilikuwepo mashine 250 tu kati ya 8000 zinazohitajika lakini akadai 7,750 zilizosalia serikali ilikuwa imeshazilipia na zinategemewa kufika nchini wiki ya kwanza ya mwezi wa tatu.

"Habari tulizo nazo siyo hata mashine zote zinafanya kazi hi sasa huko Njombe, bali ni mashine 82 tu huku nyingine zikiwa zimepelekwa kufundishia watakaoandikisha katika mikoa mingine" Amesema Freeman Mbowe Mwenyekiti wa chama kiii cha upinzani CHADEMA.

Vile vile kutokana na mashine hizo kuwa na sehemu iliyotengenezwa na bati katika eneo lake la chini zilikuwa zinapata joto, hata hivyoTume inasema changamoto hiyo imetatuliwa.

Kasoro nyingine iliyojitokeza ni mashine hizo kushindwa kutambua alama za vidole vya baadhi ya watu ambao ngozi zao za vidole zina michubuko.

Aidha, mashine hizo zimekuwa zikitumia muda mwingi kuhifadhi taarifa za mtu mmoja jambo ambalo linaleta hofu iwapo kazi hiyo itakamilika mapema na kwa ufanisi.

Lengo la kuandika wapiga kura kwa njia ya mitambo ya BVR ni kuboresha daftari la wapiga kura ambalo lilikuwa linalalamikiwa na vyama vya siasa kuwa lina upungufu mwingi ikiwamo uwezekano wa kumruhusu mtu kupiga kura zaidi ya mara moja.

Iwapo kazi hii itakamilika, kumbukumbuku zitakazohifadhiwa na mitambo hiyo zitatumika mwezi aprili wakati wa kupiga kura ya maoni ya kuamua iwapo Katiba mpya inayopendekezwa inafaa au la na baadae katika uchaguzi mkuu uanaotarajiwa mwezi oktoba mwaka huu.