Chinja chinja wa IS asema alitaka kujiua

Image caption Mohammed Emwazi

Mtu aliyejulikana kama Jihadi John alisema kuwa alitamani kujiua baada ya maafisa wa upelelezi wa Marekani kuwasiliana naye.

Mohommed Emwazi ambaye ndio 'chinja chinja' wa wapiganaji wa Islamic state na mzaliwa wa Kuwait kutoka West London alitoa matamshi hayo mwaka 2010 katika majibizano ya barua pepe na mwandishi mmoja.

Chinja Chinja huyo anasema kuwa alitaka kujiua ili kuwa mbali na maafisa hao wa M15.

Katika miezi ya hivi karibuni ,amekuwa akionekana katika kanda mbalimbali za video ambapo mateka wa Magharibi wamekuwa wakichinjwa.

Kulingana na gazeti la the Mail jumapili,Emwazi alikuwa akimtumia barua mhariri wake wa maswala ya Usalama Robert Verkaik mwaka 2010 na 2011.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mohammed Emwazi

Katika barua moja mnamo mwezi Disemba mwaka 2010,Emwazi alidai kwamba alikutana na mwanachama wa huduma ya usalama ambaye alijifanya kama mnunuzi wa tarakilishi aliyokuwa nayo.

Alishtuka baada ya mnunuzi huyo kusalimiana naye na kumtaja jina lake la kwanza ,ambalo Emwazi anasema hajamwambia mtu.

Aliandika:''nilishtuka na kuzubaa kwa sekunde chache huku mtu huyo akiondoka...nilijua ni wao!''.

Aliongezea kwamba mara nyingine hujisikia kama mfu anayetembea.