JK amuaga Captain Komba

Image caption Mamia ya watu wamejitokeza Tanzania kumuaga Captain John Komba, mbunge na msanii maarufu wa uhamasishaji aliyefariki siku ya Jumamosi.

Mamia ya watu wamejitokeza nchini Tanzania kumuaga marehemu Captain John Komba, mbunge na msanii maarufu wa uhamasishaji aliyefariki siku ya Jumamosi.

Captain Komba atakumbukwa kwa uhodari wake katika kuimba nyimbo za kuhamasisha wananchi katika mambo mbalimbali hasa ya kisiasa kwa niaba ya chama chake cha CCM.Mpaka anafariki alikuwa mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi.

Kando na siasa, Komba alishiriki katika uhamasishaji wa jamii mfano wimbo wa ‘Mgeni’ uliokuwa ukitoa elimu juu ya ugonjwa wa UKIMWI.

Mwimbaji huyo pia alihamasisha uzalendo kupitia wimbo wake wa ‘Najivunia kuwa Mtanzania’

ingawa nyimbo zinazofahamika zaidi ni nyimbo alizokiimbia chama chake kukipigia kampeni na wagombea wake wakati wa uchaguzi.

Ingawa kikundi cha Tanzania One Theatre alichokuwa akikiongoza kilikuwa maarufu kuanzia miaka ya nyuma.

Image caption Rais Kikwete akitoa heshma yake ya mwisho

Lakini umaarufu wao ulikua zaidi Captain John Komba alipotunga na kuimba nao nyimbo za kuomboleza kifo cha rais wa kwanza wa nchi hiyo Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999.

Marehemu Captain Komba alizaliwa Machi 18 mwaka 1954 mkoani Ruvuma.

Na katika maisha yake aliwahi kuwa mwanajeshi kabla ya kustaafu na kujihusisha na siasa.

Mwili wake umesafirishwa kuelekea kijiji cha Lituhi, mkoani Ruvuma ambako maziko yatafanyika siku ya Jumanne.