Boko Haram waandamwa zaidi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiongozi wa Boko Haram, Aboubakar Shekau

Majeshi kutoka Chad na Niger yameanzisha operesheni ya pamoja kaskazini mashariki mwa Nigeria dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram.

Kwa mujibu wa wakaazi wa kitongoji cha Diffa Niger, kikosi cha jeshi kimeonekana kikielekea maeneo ya mpakani mapema jana baada ya kusikika milio ya risasi.

Mashambulizi hayo makali yameanzisha vita vipya dhidi ya waislamu hao wenye msimamo mkali baada ya Umoja wa Afrika kuidhinisha uundwaji wa kikosi cha jeshi cha kanda cha wanajeshi elfu nane kupambana na Boko Haram.

Msemaji wa jeshi la Nigeria Kanali Sami Usman Kukasheka ameiambia BBC kwamba wapiganaji hao watakomeshwa.

Serikali ya Nigeria imesema kwamba mahusiano ya Boko Haram na kundi la kigaidi la Islamic State yanaonesha kwamba wapiganaji hao wa Kinigeria wako katika shinikizo.

Msemaji wa serikali ameiambia BBC kwamba kundi hilo haliko katika hali nzuri na kujivunjia hadhi ya uwezo wake kufuatia mashambulio yanayofanywa na majeshi ya Nigeria na ya kanda kwa ujumla.

Ahadi ya kundi la Boko haram, kulitii kundi la Islamic State ilitolewa siku ya Jumamosi na kiongozi wake Abubakar Shekau, katika ujumbe wa sauti uliotumwa katika mtandao wa Internet.

Kundi hilo la Boko Haram kwa miaka kadhaa sasa limesababisha machafuko, kwa madai ya kutaka kuanzisha utawala wa kiislamu kaskazini mashariki mwa Nigeria.