Mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi waja

Image caption Wadau wa uchumi

Ujumbe wa nchi za umoja wa ulaya umekutana jijini Dar es salaam Tanzania kujadiliana na wenzao wa afrika mashariki juu ya mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi unaofahamika kama EPA unaotegemewa kutiwa saini baadae mwaka huu.

Hata hivyo ushirikiano huo unaleta wasiwasi kwa baadhi ya wadau iwapo nchi za afrika mashariki zitafaidika na ushirikiano huo.

Kutoka Dar es salaam mwanahabari wetu Arnold Kayanda amehudhuria mkutano huo na hii ni taarifa yake.

Mkutano huo wenye lengo la kujadili na kufanyia kazi makubaliano yaliyomo katika mkataba wa EPA umewakutanisha wawakilishi wa umoja wa nchi za ulaya na wadau wakiwamo wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania. Miongoni mwa wafanyabiashara wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni Ali Mfuruki ambaye hadhani kama ushirikiano huu utazifaidisha nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa haziko tayari na ni bahati mbaya hatua iliyofikiwa hairuhusu kurudi nyuma maana makubaliano ya msingi yameshafanyika.

“Afrika mashariki na afrika kwa ujumla haitaweza tena kuunda msingi wa viwanda katika uchumi, baada ya muda si mrefu tutakuwa tunakula mayai ya ulaya, tunakunywa maziwa ya ulaya, tunakula kuku wa ulaya. Kwa sababu wenzetu wamejitayarisha miaka mingi sana wako tayari kufanya biashara kuliko sisi. Na sisi tumejiingiza katika hii mikataba bila kufanya matayarisho ,nina wasiwasi hata waliokuwa wanashiriki katika haya makubaliano hawakufikiria mambo haya kwa upana na undani unaotakiwa” anasema Mfuruki .

Athanassios Rammos ni afisa wa umoja wa ulaya anayehusika na nchi za afrika mashariki katika masuala ya biashara anasema utayari utakuja polepole wakati wa ushirikiano huo ukiwa umeanza kwa kuwa suala la utayari si la siku moja.

“Kutakuwa na kipindi cha mpito ambacho kitatoa muda wa kutosha kwa wazalishaji kujiandaa. Na hata hivyo ndani ya mkataba tunatoa nafasi kwa nchi za afrika mashariki kusema wakati wowote wanapoona kuna kitu hakiendi vizuri katika makubaliano” Athanassios anasisitiza.

Mazungumzo ya kufikia makubaliano ya ushirikiano huo wa kibiashara yalianza mwaka uliopita ambapo vikao kadhaa vilifanyika bila kufikia muafaka mpaka mwaka ulipita ndipo wakakubaliana. Hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kuipitia vema lugha ya mkataba na makubaliano yatakapopitishwa baadhi ya bidhaa za afrika mashariki zitaondolewa vikwazo kuingia katika nchi za umoja wa ulaya.

Takwimu za biashara za mwaka 2013 kati ya nchi za afrika mashariki na nchi za umoja wa ulaya zinaonyesha nchi za umoja wa ziliingiza afrika mashariki euro bilioni 2.2 kwa kununua bidhaa mbalimbali hususani kahawa, maua, chai, tumbaku, samaki na mbogamboga ilhali nchi za afrika mashariki ziliziingizia nchi za umoja wa ulaya bilioni 3.5 za euro kwa kununua bidhaa kama vile mitambo, vipuri, magari na dawa.