Mkenya achaguliwa makamu wa rais wa ICC

Haki miliki ya picha bb
Image caption Justice Joyce Aluoch kutoka Kenya kushoto

Majaji wa mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC wamemchagua jaji wa Kenya Joyce Aluoch kama makamu wa rais wa mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kufuatia uchaguzi huo uliofanywa siku ya jumatano,Jaji wa Argentina Silvia Fernandez de Gurmendi alichaguliwa rais wa mahakama hiyo huku jaji Kuniko Ozaki kutoka Japan akichaguliwa kama makamu wa rais wa pili.

Urais wa Mahakama hiyo unawashirikisha rais na makamu wake wawili na unatoa mwongozo wa mahakama hiyo kwa jumla.

Rais wa ICC huwa mratibu wa mahakama hiyo na idara nyengine na hutoa mawaidha kwa kiongozi wa mashtaka kuhusu maswala yanayoleta wasiwasi kwa heshima ya mahakama hiyo.

Kulingana na mkataba wa Roma ,uongozi wa mahakama hiyo ya ICC ,unasimamiwa na rais huyo bila kumshirikisha kiongozi wa mashtaka.