Mwanahabari aporwa mbele ya kamera

Haki miliki ya picha
Image caption mwandishi wa Afrika kusini aporwa akijiandaa kwenda hewani mbele ya kamera

Mwandishi maarufu wa runinga kutoka Afrika Kusini ameibiwa hadharani alipokuwa akijiandaa kwenda hewani mbele ya kamera.

Kanda ya video imewaonyesha wanaume wawili wakimvamia Vuyo Mvoko, kutoka yuninga ya taifa ya SABC ambaye alikuwa nje ya hospitali moja ya mjini Johannesburg akiripoti kuwasili kwa rais wa Zambia ili kufanyiwa ukaguzi wa matibabu.

Bwana Mvoko baadaye alisema kuwa mmoja wa wezi hao alimtishia na bunduki alipokataa kumpa simu yake ya rununu.

Wezi hao walionekana kutojali kamera zilizokuwa mbele yao.

''Sikuelewa ni kwa nini waliweza kunivamia mbele ya Kamera ilihali taa zote zilikuwa zikiwaka na kamera zilikuwa zikinasa kila kitu na, waliona kilichokuwa kikiendelea''.

Baada ya mda mfupi bwana Mvoko ambaye ni mhariri wa kituo hicho cha habari alituma ujumbe katika mtandao wake wa Twitter akisema kuwa yuko salama salmin na kutuma kanda ya video hiyo mtandaoni.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa wezi hao waliiba laptopu, na simu na kwamba maafisa walikuwa tayari wanachunguza kisa hicho.

''Tunatumaini kwamba waliotekeleza kitendo hicho watatambulika na kukamatwa'',bwana Mvoko aliiambia BBC.