Zaidi ya watu 40 wafarikii ajalini TZ

Image caption Ajali nchini Tanzania

Watu 41 wamefariki katika eneo la Changarawe, Mafinga mkoani Iringa,nyanda za juu kusini mwa Tanzania, baada ya basi la kampuni ya Majinja Express walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na Lori.

Miili ya waliofariki katika ajali hiyo imepelekwa hospitali ya Mafinga mkoani humo.

Kamanda wa polisi mkoani Iringa Ramadhani Mvungi amethibisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa kati ya hao 41 waliopoteza maisha,wanaume ni 33,wanawake watano na watoto watatu.

Akielezea chanzo cha ajali hiyo, Kamanda Mvungi amesema kuwa dereva wa Lori alijaribu kukwepa moja ya shimo katika barabara swala lililomsababisha kutoka katika upande wake wa barabara hadi upande wa basi hilo na kusababisha kugongana uso kwa uso.

Image caption Ajali nchini Tanzania

Hata hivyo kasha la lori hilo liliangukia basi hilo la kampuni ya Majinja na kusababisha vifo kwa abiria hao.

Miili ya waliofariki katika ajali hiyo imehifadhiwa katika hospitali ya Mafinga mkoani humo,na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Kwa mjibu wa kamanda mvungi taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kuhusiana na ajali hiyo.

Kumekuwa na ajali za mara kwa mara za barabarani katika nchi za Afrika mashariki ambazo husababishwa na mwendo wa kasi wa madereva na ubovu wa barabara.