300K washinikiza BBC irejeshe Top Gear

Haki miliki ya picha PA
Image caption 300K washinikiza BBC irejeshe Top Gear

Wafuasi 300,000 wa mtangazaji wa kipindi maarufu duniani ''Top Gear'' , Jeremy Clarkson wameanza kampeini ya kumnusuru baada yake kupigwa marufuku na idhaa ya habari ya BBC kwa utovu wa nidhamu.

Bwana Clarkson alisimamishwa kazi mapema jana kufuatia tuhuma za kumzaba produsa wake makonde walipokuwa wakirekodi makala yaliyotarajiwa kupeperushwa wikiendi hii.

Sasa wafuasi wake wameanzisha kampeini mtandaoni wakitaka shirika la BBC limrejeshe kazini.

Zaidi ya watu laki tatu wametia sahihi hoja hiyo yakumtaka arejee kazini huku Clarkson mwenyewe akikejeli uamuzi huo akisema huenda wakarejelea vipindi vya awali .

Mwana harakati Guido Fawkes ndiye aliyeanzisha kampeini hiyo baada ya kujulishwa kuwa kipindi chake akipendacho hakitakuwa hewani .

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mtangazji wa Top Gear jeremy alisimamishwa kazi baada ya kuzua tafrani

Clarkson, 54, alikuwa akiandaa kipindi hicho kwa pamoja na James May .

Bwana May amekana kushuhudia tafrani hiyo baina ya Clarkson na produsa wa kipindi hicho mwishoni mwa juma lililopita.

Clarkson alizua majadala mkali kwenye mitandao ya kijamii alipouliza kwanini shirika la BBC liliamua kufutilia mbali vipindi vilivyosalia

Mashabiki wake milioni 4.5 kwenye mtandao wa Twitter walifoka wakisema kuwa BBC inapaswa kumrejesha kazini kabla ya kukamilika kwa msimu wa Top Gear.