Je uliandika lini mwisho barua ya Mahaba ?

Image caption Je uliandika lini mwisho barua ya Mahaba ?

Idhaa ya utangazaji ya BBC leo imezindua mradi wa kimataifa unaohusisha wanafunzi katika utangazaji wa habari.

Wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia wamepata fursa ya kuandaa ripoti kuhusu maswala mbalilmbali yanayowahusu.

Kutoka mji mkuu wa Kenya Nairobi tunakuletea ripoti iliyoandaliwa na wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya Starehe ambapo hawaruhusiwi kubeba simu za mkononi shuleni.

Karibu katika shule ya Starehe boys centre mjini Nairobi. Shule yetu inajulikana kwa umahiri katika masomo hasa katika mitihani ya kitaifa.

Ili kuimarisha umakinifu wetu masomoni, haturuhisiwi kubeba simu shuleni.

Tuna vyumba vya computa vyenye internet lakini tunavitumia tu kwa masomo na utafiti peke yake.

Haturuhusiwi kutumia computa kwa mawasiliano kupitia barua pepe au mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter.

Lakini hilo halituzuii kuwasiliana na marafiki zetu hasa wasichana katika shule zingine.

Image caption Matumizi ya simu yamepelekea watu wengi kusahau uandishi wa barua

Inatubidi kutumia njia ya zamani,tunaandika barua,lakini sio barua za kawaida.

Ni barua zilizoandikwa kwa umakinifu na kurembeshwa kwa kalamu zenye rangi aina mbalimbali na hua tunaziandika wakati wa mapumziko.

Katika maktaba ya shule nakutana na baadhi ya marafiki zangu wakiandika barua baada ya masomo.

''Mara nyingi tunaandika barua hizi kwa marafiki zetu wasichana kwa hivyo tunaziandika kwa njia spesheli ili kupasha hisia zetu sawasawa'', anasema Charles huku akitabasamu.

Baadhi ya wanafunzi wanaamini kuandika barua ni njia bora kwani inawapa fursa kutumia vipaji vya usanii.''

Napenda sana sanaa ya uchoraji na pia matumizi ya lugha hasa ya mapenzi '', anasema Moses huku akirembesha bahasha kwa kutumia kalamu zenye rangi tofauti.

Image caption Kwa mpenzi wangu ....

''Namwandikia rafiki yangu wa karibu sana nilimuona mara ya mwisho wakati wa likizo na nahisi nimemkosa sana'', anaongeza.

Baada ya kuandika barua hizo, tarishi anatumia pikipiki yake kuzisafirisha hadi katika shule ya wasichana ya Loreto Msongari, upande mwingine wa mji.

Wasichana wanafurahia kuzipokea na baadhi yao wananieleza fikra zao kuhusu matumizi ya barua kama njia ya kuwasiliana.

''Nimependezwa sana na barua niliyopokea ,imerembeshwa kwa rangi aina mbalimbali'' anasema Stacy.

'' Nafikiri ni bora kutumia barua kuwasiliana kwasababu njia zingine kama simu zinaweza kutufanya tusizingatie masomo'', anaongeza.

Image caption Wasichana kutoka shule jirani wakisoma barua kutoka kwa wapenzi wao katika shule ya Starehe

Naye Stephanie aliniarifu kuwa alifurahishwa sana na barua aliyopokea, '' alinifurahisha sana naona alitumia lugha safi sana, naona tuendelee matumizi ya barua'', anasema.

Nilimtaka msichana Angel kunieleza kilichomvutia zaidi katika barua aliyopokea.

'' Nilifurahia pale aliponiambia kuwa nywele zangu ndefu zinapendeza na kwamba nina tabasamu ya kuvutia kiasi kwamba inaweza kumfanya awe kipofu'' anasema huku akicheka.

Huku vijana wengine duniani wakiwasiliana na marafiki zao kwa kutumia simu za mkononi imebidi sisi kutumia mbinu ya kuandika barua kufanya hivyo na inatufaa na kutufurahisha.