Janga la ebola,WHO ladaiwa kujikokota

Haki miliki ya picha AP
Image caption WHO lashtumiwa kwa kujikokota kutangaza janga la ebola

Shirika la habari la kimataifa linasema limeona nyaraka zinazoashiria kwamba huenda shirika la afya duniani lilijikokota kutangaza janga la Ebola huko Afrika magharibi, siasa ikiwa ni sehemu ya sababu.

Shirika la Associated Press linasema WHO lilitambua kuhusu uzito wa mlipuko wa ugonjwa huo mwezi Juni lakini lilisita kulitaja kuwa janga la dharura hadi ilipofika mwezi Agosti.

Linasema maafisa walikuwa na wasiwasi kwamba kwa kufanya hivyo litazikasirisha nchi zilizoathirika na kutatiza uchumi wa nchi hizo.

Kwa upande wake WHO limesema si wazi kwamba tangazo la awali lingesababisha tofauti yoyote kwa kasi ya jitihada ya usaidizi wa kimataifa.