Afisa wa upelelezi auawa Mombasa Kenya

Image caption afisa wa upelelezi

Afisaa mmoja wa upelelezi amepigwa risasi na kuuwawa katika jiji la Mombasa nchini Kenya.

Hiki ni kisa cha kwanza mwaka huu kinachogusia usalama wa eneo hilo baada ya msimu uliojaa fujo na mauaji mwaka jana.

Afisa huyo aliyekuwa akifanya kazi na idara ya upelelezi, alimiminiwa risasi akiwa ameketi na jamaa zake wawili majira ya saa tatu u nusu usiku wa Jumatano.

Kulingana na afisa mkuu wa upelelezi eneo la Pwani, bwana Henry Ondiek, watu wawili, mmoja wao akiwa amevaa buibui, walipita karibu na jamaa huyo alipokuwa akibarizi na nduguze, na ghafla wakachomoa bunduki na kum'miminia risasi kabla ya kutoweka.

Uchunguzi sasa unafanywa kung'amua madhumuni ya mauaji hayo.

Kenya imekuwa ikijitetea vikali dhidi ya taswira ya kudorora kwa usalama, ambayo imelemaza sekta ya utalii.

Siku mbili zilizopita, rais Uhuru Kenyatta aliwataka mabalozi wake kukabiliana na maoni yasiyo ya kweli kuhusu usalama.