Alshabab yaua watu 10 hotelini Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa Al Shabaab wameshambulia mkahawa mmoja mjini Mogadishu na kua watu 10

Kundi la wapiganaji linaloshukiwa kuwa sehemu ya wanamgambo wa Al Shaabab , limevamia hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Wanajeshi wa serikali ya Somali wanaendelea kupambana na wanamgambo hao waliojihami kwa vilipuzi na bunduki za rashasha.

Watu 10 wameripotiwa kuuawa katika uvamizi huu.

Kwa mujibu ya walioshuhudia wapiganaji hao wa Al Shabaab walishambulia hoteli ya Maka al-Mukarama mjini Mogadishu moja katia ya hoteli maarufu mjini humo ambayo inapendwa na wengi wa wafanyikazi wa kimataifa na mabalozi.

Aidha balozi wa Somalia nchini uswisi Yusuf Bari Bari alinusurika kifo baada ya kukwepa kupitia dirishani.

Haki miliki ya picha
Image caption Watu 10 wameripotiwa kuuawa katika uvamizi hu

Kikosi maalum cha kupambana na uvamizi wa aina hiyo kinaendelea kukabiliana na wapiganaji hao ambao wanasemekana kuwa wamebanwa katika orofa ya juu ambapo sasa wanarusha grenedi na kufyatua risasi kwa yeyote anayeonekana kuwavizia.

Afisa wa Polisi anayeongoza operesheni hiyo meja Ismail Olow ameiambia shirika la habari la Reuters kuwa kati ya wavamizi 9 waliotekeleza mashambulizi haya 6 tayari wameshauawa.

Kundi la Al Shaabab limekuwa likitekeleza mashambulizi ya aina hii katika hoteli zinazosifika kuwa mahala pa burudani kwa wageni na viongozi mashuhuri serikalini.

Shambulizi hili la leo linafuatia lingine lililoanza kwa bomu yapata mwezi mmoja uliopita nje ya hoteli hiyo.