Rubani Lubitz akipata majinamizi

Lubitz Haki miliki ya picha AFP

Mchumba wa zamani wa rubani aliyedondosha ndege kusudi katika milima ya Ufaransa ya Alps, ananukuliwa na gazeti moja la Ujerumani akisema kuwa Andreas Lubitz alikuwa akipanga njama kubwa.

Mwanamke huyo, muandalizi katika ndege, ambaye alikutana na rubani huyo kazini mwaka jana, aliliambia gazeti la

Bild kwamba rubani Lubitz alisema mara nyingi kwamba atafanya kitu ili kila mtu amkumbuke yeye ni nani.

Alimuelezea kuwa alikuwa mtu aliyekuwa akiteseka kichwani.

Mwandishi wa habari aliyemhoji dada huyo aliiambia BBC kwamba dada huyo alisema Lubitz alikuwa mtu mwema na hodari mbele ya watu, lakini faraghani alikuwa mkali hasa wakizungumzia kazi.

Anasema wakati mwengine anapata jinamizi na anaamka akipiga kelele "ndege inaanguka."

Anasema Lubitz alikasirika alipotambua hivi karibuni kwamba alikuwa hawezi kutimiza ndoto yake ya kuwa rubani kamili, kwa sababu ya ugonjwa wa akili.

Baada ya uhusiano wa siri baina yao kwa miezi mitano, dada huyo alijitenga na Lubitz kwa sababu ya hasira zake.