Mapigano makali yaendelea Yemen

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Athari ya mapigano nchini Yemen

Mapigano yameendelea katika mji wa Aden wa pili kwa ukubwa nchini Yemen, wakati waasi wa Houthi wakijaribu kutwaa udhibiti wa mji huo kutoka kwa wanamgambo wa eneo hilo.

Watu walioshuhudia tukio hilo mjini Aden wameripoti kutokea kwa mashambulio makali ya waasi, kuwepo kwa waasi walenga shabaha wakiwa juu ya mapaa ya nyumba na maiti kuzagaa mitaani.

Kuna wasiwasi wa kuongezeka kwa idadi ya watu waliojeruhiwa wakati waasi wakiendelea kusonga mbele licha ya mashambulio ya anga kufanyika kwa zaidi ya wiki moja dhidi ya majeshi ya Houthi kutoka majeshi ya washirika yanayoongozwa na Saudi Arabia.

Msemaji wa majeshi ya washirika, Ahmed Asiri, amethibitisha kuwepo mapigano makali."Sasa wanashirikiana, serikali ya mseto na jeshi la Yemen kuwazuia wapiganaji wa Houthis kudhibiti mji wa Aden. Kwa kweli hawana misaada inayoingia Aden. Majeshi yaliyokuwa yamejificha mjini Aden sasa yanasonga mbele na kuelekea Shabwa. Tunaendelea kufanya kazi kuhakikisha kuwa Aden unasafishwa haraka na kuwa salama kwa utawala wa serikali halali".

Msemaji wa shirika la misaada la Medecins sans Frontieres ameiambia BBC kuwa hospitali ya shirika hilo mjini Aden imepokea zaidi ya majeruhi 500 kutoka pande zote za mgogoro katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Jeshi la Saudi Arabia limesema katika mashambulio ya hivi karibuni, walikiharibu kikosi cha jeshi la majeshi ya Yemen chenye kushirikiana na waasi.