HABARI ZA MOJA KWA MOJA KUTOKA GARISSA

Idhaa yako ya kiswahili ya BBC imekuandalia ukurasa wa habari za moja kwa moja kufuatia shambulizi la chuo kikuu nchini Kenya.

9.00:pm:

Takriban watu 147 wengi wao wakiwa wanafunzi wameuawa katika shambulizi lililotekelezwa na kundi la Alshabaab katika chuo cha Garissa nchini Kenya .

19.24pm:

Serikali ya Kenya imetuma ujumbe katika mtandao wake wa Twitter ikisema kuwa Watu 500 wameokolewa huku 70 wakiuawa wakiwemo wapiganaji 4 wa kundi la Alshabaab #OneKenya voa CS @InteriorKE"

19.08pm:Majeruhi:

Image caption Baadhi ya majeruhi wa tukio la Chuo cha Garissa

Baadhi ya majeruhi ambao walisafirishwa kwa njia ya ndege kutoka Garissa wamewasili ili kupata matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta mjini Nairobi Kenya.

17.10pm:Rais wa Kenya:

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametuma risala za rambi rambi kwa familia za wale waliouawa katika shambulizi la chuo kikuu cha Garissa kazkazini mashariki mwa Kenya.Kiongozi huyo vilevile amewahakikishia wakenya kwamba serikali yake imechukua hatua za kuwapeleka maafisa wa usalama katika eneo hilo.Amewataka wakenya kuwa watulivu wakatu huu ambapo maafisa wa usalama wanakabiliana na wapiganaji hao.

17.00pm:Waziri wa usalama Kenya:

Waziri wa maswala ya ndani nchini Kenya Joseph Nkaiserry amethibitisha kuwa watu 15 wameuawa huku wengine 53 wakijeruhiwa kufuatia shambulizi la alfajiri katika chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya.miongoni mwa waliokfariki ni walinzi wawili wa mlango wa chuo hicho.Akizungumza kutoka Garissa Nkaiserry amesema kuwa oparesheni ya kuwasaka wahalifu hao itaendelea hadi mateka wote waokolewe.

16.50pm:Mshukiwa mkuu:

Serikali ya Kenya imemtaja Mohammed Kuno kama mshukiwa mkuu aliyepanga njama za shambulizi la chuo kikuu mjini Garissa.Katika taarifa kwa vyombo vya habari waziri wa usalama nchini Kenya Joseph Nkaiserry alitoa zawadi ya dola 53,000 kwa mtu yeyote atakayemkamata mshukiwa huyo ama kutoa habari zake.Kuno anajulikana kama 'Gama'adhere kwa jina maarufu.

15.10pm:Mitandaoni:

Image caption Chuo kikuu cha Garissa

Mwandishi wa habari wa Kenya Dennis Okari ambaye yuko katika eneo la chuo kikuu cha Garissa ameandika katika mtandao wake wa Twitter akisema kuwa:Wapiganaji hao wako katika jumba la kulala wanafunzi .''ninaweza kusikia milio ya risasi kutoka upande wa pili.@ntvkenya".

14.48pm:Mahitaji ya Damu:

Image caption kituo cha kutoa damu mjini Garissa

Kufuatia shambulizi la chuo kikuu cha Garissa ,Shirika la msalaba mwekundu Red Cross limewataka raia wa Garissa kutoa msaada wa damu.Walioitikia wito huo tayari wameeleka katika hospitali kuu ya Garissa mbapo kituo cha kutoa damu kilianzishwa chini ya mti.

14.40pm:Shahidi wa shambulizi:

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Garissa Collins Wetangula amesema kuwa wakati wapiganaji hao walipoingia katika nyumba anayolala aliwasikia wakifungua milango na kuwauliza watu iwapo ni waislamu ama wakristo.''kama wewe ni mkristo unapigwa risasi papo hapo.kila mlio wa risasi nilipousikia nilidhani nitauawa'',aliambia shirika la habari la AP.Amesema kwamba maafisa wa usalama baadaye waliingia kupitia dirisha moja na kumtoa yeye na wenzake hadi katika eneo salama.

14.30pm:Maafisa wa matibabu kwa sasa wanaelekea katika hospitali ya kuu ya Garissa nchini Kenya ili kusaidia wale waliojeruhiwa

14.00pm:Kwa ufupi

Image caption Ramani ya chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya

Takriban watu 15 wanaodaiwa kufinika nyuso zao wameshambulia chuo kikuu cha Garrissa Kaskazini mashariki mwa Kenya.

Watu hao wanaodaiwa kuingia katika taasisi hiyo mwendo wa saa kumi asubuhi wakati ambapo waislamu walikuwa wakifanya sala yao ya alfajiri.

Hatahivyo maafisa wa polisi wanasema kuwa shambulizi hilo lilifanyika mwendo wa saa kumi na moja unusu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption wanafunzi wa chuo kikuu cha Garissa

Mwandishi wa BBC mjini humo anasema kuwa walinzi wawili waliuawa katika lango la chuo hicho huku maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda chuo hicho pamoja na wanafunzi wakijeruhiwa.

Walioshuhudia wanasema kuwa kumekuwa na majeruhi mengi ndani ya chuo hicho.

Mwandishi wetu anasema kuwa wapiganaji hao bado wako ndani ya chuo hicho na wamewateka nyara watu kadhaa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho waliosalimika

Jeshi la Kenya KDF ,maafisa wa polisi na amabulansi wamefika katika eneo la tukio na sasa wameingia ndani ya majengo ya chuo hicho ambapo kumekuwa na ufyatulianaji wa risasi kati ya washambuliaji na maafisa wa jeshi.

13.40pm:Waislamu na wakristo waliotekwa ndani ya Jumba hilo la Chuo kikuu cha garissa wamedaiwa kutawanywa kabla ya waislamu 15 kuwachiliwa huru kulingana na msemaji wa kundi hilo la Alshabaab.

13.35pm:Serikali ya kenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anatarajiwa kulihutubia taifa kufuatia shambulizi hilo la chuo kikuu cha Garrisa mapema leo.

13.30pm:Alshabaab:

Image caption Maafisa wa Polisi wa kenya

kundi la wapiganaji wa Alshabaab limesema kuwa liko ndani ya Chuo hicho kikuu na limewatawanya waislamu na wakristo

13.20pm:Wapiganaji wamedaiwa kuwateka nyara wanafunzi na kuwaua watu 14 katika chuo hicho kulingana na wafanyikazi wa msaada na maafisa wa polisi.Takriban watu 65 wengine wamejeruhiwa baada ya washambuliaji kuvamia chuo hicho.Vituo vya habari nchini kenya hatahivyo vinaiweka idadi hiyo kuwa watu 16.

13.05pm:Idadi ya watu waliouawa kufuatia shambulizi la wapiganaji wa kundi la alshabaab imefikia 14

13.03pm:Al shabaab

Haki miliki ya picha AP
Image caption Alshabaab lakiri kutekeleza shambulizi

Kundi la wapiganaji wa Al-shabaab limekiri kutekeleza shambulizi katika chuo kikuu cha Garissa Kaskazini mashariki mwa Kenya huku likiwaua watu 14

12.47pm:Wanafunzi

Image caption wanafunzi wa chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya

Chuo hicho cha Garissa kina takriban wanafunzi 1000, na wafanyikazi wengine.

12.30pm Wanafunzi:

Image caption Wanafunzi waliodaiwa kutoroka

Baadhi ya wanafunzi wamedaiwa kutoroka kutoka mabweni waliokuwa wakilala

12.20pm:Wapiganaji

Image caption Wapiganaji

Wapiganaji hao wanaodaiwa kuwa watano wanaaminika kuwa ndani ya jengo hilo la Chuo kikuu .

12.18pm:Kenya Red Cross

Image caption Maafisa wa polisi wakikabiliana na wapiganaji huko Garissa kenya

Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya linasema kuwa watu 30 wamejeruhiwa huku wanne kati yao wakiwa na majeraha mabaya..Kwa sasa shirika hilo linawasafirisha madaktari katika eneo hilo.

11.30am Idadi ya watu waliouawa kufuatia shambulizi la chuo kikuu cha Garrissa Kaskazini mashariki mwa Kenya imefikia watu sita huku wengine 29 wakidaiwa kujeruhiwa.