Vita vikali vyaendelea kusini mwa Yemen

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Yemen

Duru kutoka Yemen zasema kuwa makabiliano makali kati ya waasi wa Houthi na wanajeshi walio watiifu kwa rais wa Yemen Abd Rabbu Mansour Hadi, yanaendelea kusini mwa nchi hiyo katika mji wa Aden.

Ndege moja ya kijeshi ya Saudi Arabia imetekeleza mashambulizi makali katika ngome ya Houthi viungani mwa mji wa Aden.

Inakisiwa kwamba zaidi ya watu hamsini wameuawa katika makabiliano makali mjini humo katika kipindi cha masaa ishirini na manne yaliyopita.

Majeshi ya muungano yakiongozwa na Saudi Arabia kwa siku ya kumi na moja leo Jumatatu, yanaendelea kushambulia ngome za wapiganaji wa Houthi.

Kusini mwa Yemen waasi wa Huthi wamepata mafanikio zaidi dhidi ya wanajeshi watiifu kwa Rais Abdrabbuh Mansur Hadi, kwenye mji wa Aden, licha ya kuendelea kwa mashamambulizi ya angani.

Kazkazini zaidi mwa nchi hiyo, ndege za majeshi ya muungano zimeendelea kushambulia maeneo karibu na mji mkuu Sanaa.