John Kerry aionya Iran kuhusu Yemen

Haki miliki ya picha AP
Image caption John Kerry na Javad Zarif wa Iran

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry ameionya Iran dhidi ya hatua yake ya kuwaunga mkono wapiganaji wa Houthi wanaopambana na serikali ya Yemen.

Katika mahojiano ya Televisheni, John Kerry amesema Marekani itaiunga mkono nchi yoyote mashariki ya Kati itakayotishiwa na Iran.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Iran na Marekani

Jana Iran ilituma meli mbili za kivita katika bandari ya Aden kuwaunga mkono waasi, ambao wanapambana kuudhibiti mji huo.

Marekani inaunga mkono muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia ambalo lengo lake kuu ni kuwafurusha waasi hao na kurudisha utawala wa rais Abdrabbuh Mansour Hadi ambaye alilitoroka taifa hilo mwezi uliopita.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mkutano kati ya Iran na viongozi wa mataifa sita bora duniani

Hatahivyo Iran imekana madai kwamba inawapatia usaidizi wa kijeshi waasi hao wa Houthi.

Wakati huohuo, raia wa Comoro wapatao 42 wanaoishi Yemen wamekwama nchini humo.

Balozi wa Comoro ameiomba Qatar isaidie kuwahamisha, lakini nchi hiyo imelipeleka ombi hilo kwa Saudi Arabia.

Kuna mpango sasa wa kuwahamisha Wacomoro hao kwa njia ya barabara, lakini kufanya hivyo kuna hatari zake.