Wazozania 'BBC' India

Image caption Borivali Biryani Centre

Kampuni mbili za kuuza chakula katika mji wa India wa Mumbai zimeenda mahakamani kupigania utumizi wa jina BBC kwa ufupi.

Kampuni hizo ni Borivali Biryani Centre inayodai kuwa mmiliki halisi wa BBC na kwamba Bombay Baking Company iliiba jina hilo.

Msemaji wa Biryani Centre amesema kuwa hajali kwamba jina hilo linatumiwa na kituo kimoja kikuu cha habari.

''Hiyo ni kwa ukubwa tu, lakini hapa India sisi ndio BBC''.Kituo hicho cha Biryani kinataka kulipwa dola laki moja kufidia hasara wanayopata.

Image caption Bombay Baking Company

Lakini kampuni hiyo ya kutengeza mikate na keki inasema kuwa haioni tatizo lipo wapi.

Msemaji wa kampuni hiyo iliopo katika hoteli ya JW Marriot hakutaka kuingizwa katika mjadala wa iwapo ni haki kutumia jina BBC.

Lakini shirika la BBC mjini London limesema kuwa halitatoa tamko lake kuhusu kesi hiyo.

Chanzo cha kesi hiyo ambayo inasikizwa na mahakama ya Bombay ni kwamba kampuni zote hutumia neno ''Hello BBC'' wanapopokea simu kuchukua maagizo ya chakula kutoka kwa wateja wao.