Polisi wanasa kilo 2 za Heroin Kenya

Image caption Afisa mkuu wa polisi mjini Mombasa Robert Kitur aliyeongoza operesheni hiyo

Polisi nchini Kenya wanazuilia mashua moja inayoshukiwa kuwa na madawa ya kulevya.

Aidha watu watano wamekamatwa baada ya kupatikana na kilo mbili za mihadarati aina ya heroin, huku raia mmoja wa Uingereza akisakawa kujibu maswali.

Msako huu ulianza wiki iliyopita baada ya polisi kupata ripoti ya ulanguzi wa madawa ya kulevya mjini Kilifi, kilomita 70 Kaskazini mwa Mombasa.

Polisi waliliandama gari moja dogo hadi Bandari ya Kilifi

Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi mjini Mombasa, bwana Robert Kitur, gari hilo lilipatikana na kilo mbili za madawa ya heroine, iliyo na thamani ya karibu dola 65,000.

''tulivizia gari moja ambayo tulikuwa na ufahamu kuwa ilikuwa na walanguzi wa madawa ya kulevwa na tulipoipekua tulipata kuwa walikuwa na karibu kilo 2 za Heroin'' alisema afisa mkuu wa polisi wa Mombasa Robert Kitur.

Inaaminika kuwa madawa hayo yalikuwa yasafirishwe hadi Kisiwa cha ushelisheli au mjini Dar-es-Salaam .

Image caption Boti la jeshi la wanamaji la Kenya lililoongoza operesheni kuinasa boti linalomilikiwa na raia muingereza

Nahodha wa mashua hiyo, raia wa ushelisheli, anazuiliwa pamoja na wakenya watatu waliopatikana ndani ya boti hilo.

Kwa wakati huu polisi wanamtafuta mmiliki wa mshua hiyo ambaye anasemekana kuwa ni raia wa Uingereza.

Kwa sasa tumefanya uchunguzi wa kimsingi na tumegundua kuwa boti hili linamilikiwa na bwana mmoja anayetambulika kama Mike Connel ambaye ni raia wa uingereza'' aliongezea Kitur.

Maafisa wa usalama wanaizuilia mashua hiyo katika bandari ya Mombasa, huku wanamaji wa Kenya Navy wakishika doria katika eneo hilo.

Pia uchunguzi unaendelea kubainisha kama kuna madawa zaidi ndani ya boti.