Waliojiunga Al Shabab wajisalimishe

Haki miliki ya picha AP
Image caption Serikali ya Kenya imetoa makataa ya siku 10 kwa wale wote waliojiunga na kundi la Al Shabaab kujitokeza na kusamehewa

Serikali ya Kenya imeahidi kuwasamehe wakenya ambao wamepokea mafunzo ya kigaidi endapo watajitokeza katika kipindi cha siku 10 zijazo.

Waziri wa usalama wa ndani jenerali mstaafu Joseph Nkaissery pia amewaonya wazazi wa vijana kama hao kwamba watachukuliwa hatua kali endapo hawataijulisha serikali kuhusu kujiunga kwa wanao na kundi la Al Shabaab.

Serikali imewapa wale wote waliopokea mafunzo kutoka kwa Al Shabaab siku kumi kupiga ripoti kwa afisi za wasimamizi wa miji ya Garissa, Mombasa ama Nairobi.

Haki miliki ya picha epa
Image caption Kenya imechapisha nambari za simu ambazo wakenya wanaweza kutumia kutoa ripoti hizo kisiri kuhusu Al Shabaab

Waziri huyo wa usalama pia amechapisha nambari za simu ambazo vijana hao wanaweza kutumia kutoa ripoti hizo kisiri.

Amesema wale watakaoitikia mwito wake watasamehewa na kupata usaidizi wa kurejea katika jamii.

Hata hivyo amewaonya wale ambao hawatafanya hivyo katika siku kumi zijazo kwamba serikali itakabiliana nao kama wahalifu kwa mujibu wa sheria za Kenya.

Image caption Al Shabaab ilikiri kutekeleza shambuliz ambalo wakristo 147 waliuawa katika chuo kikuu cha Garissa

Wazazi ambao wanao wametoweka, au wanaojua kuwa wamejiunga na Al Shabaab ama kuuwawa nchini Somalia wametakiwa kutoa ripoti hizo kwa serikali la sivyo wafunguliwe mashtaka kama washiriki wa magaidi.

Hofu imeibuka nchini Kenya baada ya ripoti kwamba mmoja wa wanamgambo walioshambulia chuo kikuu cha Garissa na kuchangia kuwaua watu 147 alikuwa Mkenya aliyesomea taaluma ya sheria jijini Nairobi.

Babake, ambaye ni chifu, alipiga ripoti kwa serikali alipotoweka mwanawe miaka miwili iliyopita.