18 waaga katika ajali Tanzania

Image caption Watu wasiopungua 18 wameuawa katika ajali ya gari mkoa wa Mbeya kusini magharibi mwa Tanzania

Watu wasiopungua 18 wameuawa katika ajali ya gari mkoa wa Mbeya Kusini Magharibi mwa Tanzania baada ya basi dogo la abiria kuanguka na kutumbukia kwenye bonde lenye maji.

Mwandishi mmoja wa habari aliyefika eneo la ajali ameeleza kuwa basi hilo dogo limetumbukia bondeni katika eneo lenye mteremko mkali na kona.

Polisi wanachunguza chanzo cha ajali, lakini walioshuhudia wanadai dereva wa gari hilo alikuwa akiwakimbia madereva wengine

waliotaka kumlazimisha aunge mkono mgomo wa utoaji huduma unaoendelea kwa safari za kati ya Mbeya na Kyela.

Imeelezwa kuwa madereva wa mabasi ambayo kwa kawaida hutoa huduma kati ya eneo la Kyela na Mbeya mjini walikuwa katika mgomo,

na kwamba hawakufurahishwa na basi hilo dogo kuendelea kutoa huduma ndipo wakawa wanamfukuza hatimaye akashindwa kulidhibiti

Ajali hiyo ni mwendelezo wa ajali mbaya za barabarani kuhusisha magari ya abiria ambazo zimetokea Tanzania kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita.