Watu zaidi ya 30 wauawa Afghanistan

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Eneo kulikotokea shambulizi

Shambulizi la kujitoa mhanga kwenye mji ulio mashariki mwa Afghanistan wa Jalalabad limewaua watu 33 na kuwajeruhiwa karibu wengine 100.

Ripoti zinasema kuwa shambulizi hilo lilitokea karibu na benki ambapo wafanyikazi wa serikali wanalipwa misharaha yao.

Maafisa wanasema kuwa mtu aliyeendesha shambulizi hilo alikuwa na pikipiki.

Kulitokea shambulizi la pili karibu na madhabahu mjini Jalalabad lakini haijulikani kama kulikuwa na madhara yoyote.

Hakuna kundi lililokiri kuhusika, lakini mji wa Jalalabad umekuwa ukilengwa kila mara na kundi la Taliban.