Mawaziri wa EU wajadali kuhusu wahamiaji

Image caption Mkuu wa sera za Ulaya Federica Mogherini

Mkuu wa sera kwenye Muungano wa Ulaya anasema kuwa Ulaya ina wajibu wa kuchukua hatua ili kukabiliana na hali inayozidi kuwa mbaya kuhusu wahamiaji kwenye bahari ya Mediterranean.

Federica Mogherini alikuwa akizungumza kabla ya mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Muungano wa Ulaya kuzungumzia hali ya wahamiaji kutoka afrika wanaovuka bahari ya mediterranean.

Siku ya Jumamosi mamia ya wahamiaji wanaaminika kuzama baada ya mashua yao kupinduka nje ya pwani ya Libya.

Haki miliki ya picha AFP Getty Images
Image caption Wahamiaji wakiwa baharini

Idadi kamili ya watu walioaga dunia haijulikani. Eneo ambapo mashua hiyo ilizama lina kina kirefu na huenda abiria wengi walikuwa wamefungiwa ndani ya mashua.

Umoja wa mataifa unasema kuwa njia kutoka kaskazini mwa afrika kwenda Italia na Malta imekuwa eneo hatari zaidi duniani na makundi ya uokoaji yanastahili kuwa yanapiga doria eneo hilo.

Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi anasema kuwa mkutano wa dharura unahitajika kuandaliwa ili kuzungumzia suala hilo.