Jeshi limefanya shambulio la anga Sanaa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Eneo lililoshambuliwa Sanaa

Wakaazi wa mji mkuu wa Yemen, Sanaa, wamesema kumekuwa na mlipuko mkubwa, kufuatia shambulio la anga yaliyofanywa na wanajeshi wa muungano wanaoongozwa na Saudi Arabia.

Moshi mkubwa ulitanda katika anga za mji wa Sanna, katika kile wakaazi wa mji huo wanasema kuwa ni shambulio kubwa zaidi kuwahi kufanywa na wanajeshi hao wa muungano, dhidi ya waasi wa Houthi na washirika wao.

Wanajeshi hao walikuwa wakilenga kituo kimoja cha kuhamisha cha kurusha makombora, ambacho kimeshambuliwa kwa mara kadhaa.

Madirisha ya vyumba katika sehemu nyingi ya mji huo yaliharibiwa kwenye mlipuko huo na wakaazi kadhaa wamechapisha uharibifu uliosababishwa kwenye mtandao wa Twitter.

Ripoti zinasema watu kadhaa wamejeruhiwa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wapiganaji wa waasi wa Houthi

Wanajeshi hao wa muungano wameimarisha mashambulio ya anga dhidi ya waasi hao katika siku za hivi karibuni, huku mapigano kati ya waasi na makundi mengine yakiendelea, hasa katika mji wa bandari ya Kusini wa Aden.

Wakati huo huo madaktari katika mji wa kusini wa Aden, wameiambia BBC kuwa wagonjwa wengi wanafariki kwa sababu ya kukosa matibabu.

Hospitali zinaishiwa na bidhaa muhimu za matibabu wakati mapigano kati ya vikosi vya seriali vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia na waasi wa Shia wa Houthi yanapochacha.

Mwandishi wa BBC ambaye alizuru mji huo aliambiwa kuwa wagonjwa walikuwa wakifa kwa sababu hawangeweza kutibiwa kwa njia inayofaa.

Makundi ya kutoa huduma za matibabu yamelemewa na idadi ya wagonjwa wanaolazwa na yametoa wito kwa madawa zaidi na vifaa vingine vya matibau.

Kiongozi wa waasi amekashifu Saudi Arabia kwa kujaribu kuivamia na kuiteka nchi ya Yemen.