Ethiopia yaomboleza vifo vya Raia wake

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raia wa Ethiopia takriban zaidi ya 20 waliuawa kinyama na Wanamgambo wa Islamic State

Ethiopia imeanza siku tatu za maombolezo ya raia wake zaidi ya ishirini waliouawa kinyama na magaidi wa Islamic State nchini Libya. Jamaa wameeleza mshtuko wao baada ya kutazama video inayoonyesha jinsi wapendwa wao walivyouawa.

Jamaa na marafiki walikusanyika mjini Addis Ababa kuwakumbuka wependwa wao zaidi ya ishirini waliouwawa kikatili. Walitoka Ethiopia kutafuta maisha mazuri, lakini wakaangamia kwenye Ufuo wa bahari za Libya.

Wanamgambo wa Islamic State waliwakamata wakiwa safarini kueleka barani Ulaya, wakawapiga risasi na kuwachinja kwenye ufuo wa bahari ya Mediterranean, na kupeperusha mauaji hayo kwenye mitandao.

Waethiopia wengi wako katika hali ya mshtuko kwa jinsi wenzao walivyopoteza maisha. Taifa hilo lilianza majonzi ya siku tatu kuanzia Jumanne, huku maombi yakiendeshwa na Viongozi wa dini ya kikristo na Kiislamu.

Mmoja wa wale waliotekeleza unyama huo kwenye video hiyo amenukuliwa akiwaonya wakristo kugeuka na kuwa waisilamu au wafe. Lakini Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alitoa wito wa muungano na umoja wakati huu wa maombolezo.

Desalegn alisema wapiganaji hao wanadhamiria kuangamiza utu, na kuwahimiza wananchi wake kukabiliana nao kwa pamoja bila kuzingatia dini. Sheikh Mohammed Jemal, Mkuu wa Baraza la Maslahi ya Kiislamu nchini Ethiopia, amenukuliwa na shirika la habari la ufaransa AFP akisema kwamba kuwaua watu kama kuku haikubaliki Kiislamu.

Serikali ya Ethiopia imeapa kulipiza kisasi, huku waziri wa Maswala ya Kigeni Tedros Adhanom akisema taifa hilo litakabiliana vikali na wanamgambo hao kufuatia mauaji hayo. Huku hayo yakijiri, taarifa zinasema kuwa baadhi ya waliouawa huenda wakawa raia wa Eritrea. Gazeti moja nchini Israel limeripoti kuwa waathiriwa watatu kwenye video ni raia wa Eritrea walionyimwa ukimbizi Israel.