Wahamiaji wazidi kuokolewa Italia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wahamiaji wakiwa wameokolewa na walinzi wa pwani ya Italia katika bahari ya Mediterani

Walinzi wa pwani ya Italia wamesema karibu wahamiaji elfu sita waliokuwa wakijaribu kufika Ulaya wameokolewa kutoka bahari ya Mediterani tangu Jumamosi asubuhi.

Msemaji wa walinzi wa pwani ya Italia ameiambia BBC kuwa vikosi kumi na saba vya uokoaji vinaendelea na kazi hiyo, katika kile kinachosemekana kuwa operesheni kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika na ya aina yake kufanyika mwaka huu.

Mapema Jumamosi meli za Italia ziligundua miili ya watu kumi kutoka nje ya pwani ya Libya. Ongezeko la watu kujaribu kuvuka bahari limetokana na watu wanaofanyabiashara ya kuvusha watu kwa njia ya magendo kutumia mwanya wa hali ya utulivu wa bahari.

Mwezi uliopita Umoja wa Ulaya walikubaliana kuongezeka operesheni za utafutaji na uokoaji kufuatia vifo vya zaidi ya watu mia nane kutoka meli moja iliyokuwa imezama katika bahari ya Mediterani.