Juventus yaichapa Real Madrid 2-1 UEFA

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wachezaji wa timu ya Juventus wakishangilia baada ya kuibwaga Real Madrid 2-1 katika mchezo wa nusu fainali za UEFA

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali za Kombe la Mabingwa barani Ulaya kati ya Juventus ya Italia dhidi ya Real Madrid ya Hispania umefanyika Jumanne usiku kwa Juve kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Juventus wenyeji wa pambano hilo walipata bao lao la kwanza katika dakika ya 8 ya mchezo kupitia kwa Alvaro Morata. Hata hivyo Cristiano Ronaldo alisawazisha katika dakika ya 27. Matokeo yaliyodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Juventus walipata goli tena katika dakika ya 57, kutokana na mpira wa adhabu ya penalti, ambapo Carlos Tevez aliifungia timu yake. Hadi kipenga cha mwisho, Juventus 2, Real Madrid mabingwa watetezi 1. Timu hizo zitarudiana tarehe 13 Mei katika uwanja wa Bernabeu, mjini Madrid.

Katika pambano lingine la nusu fainali za Kombe la UEFA, timu nyingine ya Hispania, Barcelona wanawaalika Bayern Munich ya Ujerumani Jumatano usiku katika uwanja wa Nou Camp. Barcelona itakuwa na kibarua kigumu kuwaangusha Bayern ambayo kwa sasa inafundishwa na kocha wake wa zamani Pep Guardiola.