Rais Sirleaf afurahi Ebola imekwisha

Rais Ellen Johsnon Sirleaf Haki miliki ya picha Getty

Shirika la Afya Duniani, WHO, imetangaza rasmi kwamba hakuna tena Ebola nchini Liberia.

Taarifa ya WHO inasema kuwa nchi hiyo haikupata mgonjwa wa Ebola kwa siku 42.

Kabla ya kupanda basi kutembea mjini Monrovia kusherehekea kumalizika kwa ebola nchini, rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, alisoma taarifa kwa BBC ambapo aliuambia ulimwengu kwamba amefurahi kuwa ugonjwa huo umefyekwa nchini.

Rais Sirleaf amesema nchi yake imepoteza watu wengi wema na waliokuwa na jitihada.

Na alitaka nchi ziwe macho na mifumo ya afya lazima iimarishwe:

"Ni jukumu letu kwa kizazi kijacho katika nchi zote zinazoendelea kujenga miundo mbinu ya afya inayofanya kazi, mifumo ya afya ambayo haitoacha watu wakiugua au kufa barabarani.

Tumepiga hatua kweli Liberia katika miaka kumi iliyopita lakini haikutosha na lazima tujitahidi zaidi.

Hiyo inamaanisha hospitali zenye zana sawasawa, kufunza madaktari na wauguzi wa kutosha, na barabara zinazofaa kusafirisha vifaa kwa watu wanaohitaji."