Afrika Kusini yawatimua wageni 400

Haki miliki ya picha
Image caption Afrika Kusini yawatimua wageni 400

Afrika Kusini imeanzisha operesheni ya kuwafurusha raia wa mataifa mengine ya Afrika kufuatia vurumai za kibaguzi zilizoibuka dhidi ya wageni katika taifa hilo hivi majuzi.

Zaidi ya wageni 400 kutoka Msumbiji walikuwa katika kundi la kwanza kufukuzwa.

Afrika Kusini imechukua hatua hiyo baada ya vurumai ya kibaguzi dhidi ya wageni iliyopelekea watu saba raia wa kigeni kuuawa na wenyeji waliokuwa wakilalama kuwa wamechukua nafasi zao za kazi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wa Afrika Kusini wakiwafurusha wageni mjini Durban

Mapigano hayo ya kibaguzi yalitibuka katika miji ya Durban na Johannesburg wenyeji walipoanza kuwavamia wageni pamoja na kuwapora mali yao.

Serikali ya Msumbiji imeshangazwa na hatua hiyo ya kuwaondoa raia wake kwa nguvu huku waziri wake wa maswala ya kigeni Oldemiro Baloi akisema alikuwa anatarajia kufanya mazungumzo na mwenzake wa Afrika Kusini.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption ''Operesheni Fiela'' kama inavyofahamika ilipelekea watu zaidi ya 889 kukamatwa.

Waziri huo alisema haelewi kwa nini raia wa Msumbiji wanakamatwa na kuondolewa nchini humo kwa nguvu ilhali swala hilo lilikuwa linashughulikiwa baina ya serikali hizo mbili.

Mwandishi wa BBC Nomsa Maseko aliyeko huko anasema hatua hii ya serikali imewashangaza wengi hususan baada ya serikali kupewa ilani ya mahakama dhidi ya kuwakamata na kuwafukuza wageni.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Zaidi ya wageni 400 kutoka Msumbiji walikuwa katika kundi la kwanza kufukuzwa.

Operesheni hiyo ya kuwakamata wageni imekuwa ikiendeshwa majira ya alfajiri hasa katika mitaa duni ya miji ya Durban na Johannesburg.

''Operesheni Fiela'' kama inavyofahamika ilipelekea watu zaidi ya 889 kukamatwa.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu walikwenda mahakamani kupinga operesheni Fiela wakisema inahalalisha vita vya kibaguzi vilivyo sababisha vifo vya watu saba wengi wao wakiwa raia wa mataifa ya Afrika.