Rais Mutharika amlilia mwandishi wa BBC

Image caption Rais wa Malawi Peter Mutharika

Rais Peter Mutharika wa Malawi ametoa salaam za rambirambi kufuatia kifo cha mwandishi wa habari wa BBC nchini humo Raphael Tenthani, ambaye amekufa katika ajali ya gari.

Bwana Mutharika amesema, Tenthani atakumbukwa kama mtu mwenye kipaji cha hali ya juu, mcheshi na mchangamfu.

Raphael Tenthani ambaye alikuwa na umri wa miaka 43 alifahamika nchini kote Malawi na amekuwa akiripotia Idhaa ya Kiingereza ya BBC kwa zaidi ya miaka kumi. Pia alifanya kazi na shirika la habari la Marekani la Associated Press. Mwaka 2010 alishinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Vyombo vya Habari kwa kazi yake kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia.