Wapiganaji washia waelekea Ramadi, Iraq

Image caption Ramadi

Inasemekana kuwa wapiganaji wa kishia wanadaiwa kuelekea Ramadi, mji mkuu wa mkoa wa Al-Anbar, Magharibi mwa Baghdad, kufuatia kutekwa kwake na wapiganaji wa kundi la Islamic State mnamo Jumapili.

Mji huo ulinyakuliwa na Islamic State licha ya kuimarishwa kwa mashambulizi ya ndege za kijeshi na Marekani na mataifa washiriki wake.

Waziri wa Ulinzi wa Iran pia yuko Baghdad leo kufanya mashauriano na maafisa wa Serikali nchini humo.

Kutimuliwa kwa wanajeshi wa Iraq kumemlazimisha Waziri Mkuu wa taifa hilo kufanya kile ambacho hakutaka kufanya.

Image caption Ramadi

Ilibidi ayaombe makundi ya upinzani ya kishia yanayoungwa mkono na Iran, kusaidia kukomboa Ramadi, licha ya uhasama unaoweza kutokea kufuatia kuwatumia wapiganaji wa Kishia katika maeneo yanayojulikana kuwa ngome za Wasuni.

Kuna ripoti kuwa makundi ya wapiganaji ambayo tayari yako katika eneo hilo yamekaribia Ramadi, na yanaendelea kunoa makali yao ili kuwatimua wanachama wa Islamic State katika mji huo muhimu.

Wamarekani wamejikuta katika njia panda kutokana na utekaji wa mji wa Ramadi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption ramadi

Walishambulia na ndege za kivita ili kuwasaidia wanajeshi wa Iraq kushikilia mji wa Ramadi lakini ukweli ni kwamba wao hawakuwa na moyo wa kupambana kikamilifu na wapiganaji hao wa Islamic State.

Wachanganuzi wanajiuliza sasa kama iwapo Marekani itaendelea kutumia ndege hizo hizo kukabiliana na Islamic State wakati ambapo wapiganaji waliolenga kwenda Ramandi ni wale wanaoungwa mkono na Iran.