Saudia:Nafasi 8 za kutekeleza hukumu ya kifo

Image caption Saudi Arabia imetangaza nafasi 8 za watu ambao kazi yao itakuwa ni kutekeleza hukumu ya kifo!

Je unatafuta kazi ?

Saudi Arabia imetangaza nafasi 8 za watu ambao kazi yao itakuwa ni kutekeleza hukumu ya kifo!

Amini usiamini taifa hilo linatarajia ongezeko la hukumu ya kifo na hivyo inajiandaa kwa kuongeza nafasi ya watu watakotia wahalifu kitanzi.

Nchini humo hukumu ya kifo hutekelezwa hadharani mtuhumiwa anapokatwa kichwa mbele ya umma.

Kazi hii hata hivyo haihitaji tajriba ya aina yeyote.

Majukumu yako yatakuwa kuua kwa upanga na wakati mwengine kuwakata mikono watu watakaopatikana na makosa madogo madogo.

Nafasi hizo nane za kazi zilitangazwa katika mtandao wa serikali unaotangaza kazi za umma

Taifa hilo la Kiislamu ni miongoni mwa mataifa matano yenye kutekeleza hukumu nyingi zaidi ya kifo duniani.

Saudia iliorodheshwa katika nafasi ya tatu mwaka wa 2014 nyuma ya China na Iran.

Iraq inashikilia nafasi ya nne huku Marekani ikifunga orodha hiyo ya mataifa tano, hii ni kwa mujibu wa takwimu ya shirika la kipigania haki za kibinadamu la Amnesty International.

Image caption Mwaka uliopita Watu 88 walihukumiwa kifo kwa mujibu wa Human Rights Watch (HRW).

Mwanamume mmoja aliyechinjwa siku ya jumapili alikuwa mtu wa 85 kunyongwa mwaka huu kwa mujibu wa shirika la habari la Saudia.

Mwaka uliopita Watu 88 walihukumiwa kifo kwa mujibu wa Human Rights Watch (HRW).

Amnesty kwa upande wake ilichapisha takwimu zilizoonesha kuwa watu 90 walihukumiwa kifo mwaka jana.

Asili mia kubwa ya wale waliohukumiwa kufa walikuwa wameua huku 38 kati yao wakihukumiwa kwa kuhusika na mihadarati.

Takriban nusu ya idadi hiyo ilikuwa ni raia ya Saudia huku wengine wakiwa ni raia wa Pakistan, Yemen, Syria, Jordan, India, Indonesia, Burma, Chad, Eritrea Ufilipino na Sudan.

Maafisa wakuu serikalini hawajaeleza kwanini idadi ya hukumu ya kifo imeongezeka maradufu hata hivyo wanadiplomasia wanasema kuwa ongezeko hilo limetokana na ongezeko la majaji walioapishwa hivi majuzi.

Wachanganuzi wa maswala ya kimataifa hata hivyo wanahoji mbinu hiyo ya utawala nchini humo kutumia sheria kali kukabili matatizo mengi yanayokumba eneo hilo.

Saudi Arabia inaendeleza kampeini dhidi ya waasi waHouthi kutoka Yemen.