Burundi: rais aonekana akicheza licha ya maandamano

Image caption Burundi: rais aonekana akicheza licha ya maandamano

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ameonekana akicheza mpira pamoja na marafiki zake mjini Bujumbura licha ya mgogora wa kisiasa nchini mwake.

Image caption Rais Nkurunziza ni kocha aliyehitimu

Rais Nkurunziza,alikuwa akisakata kabumbu ndani ya mji mkuu wa Bujumbura mji uliokumbwa na maandamano makubwa tangu atangaze nia ya kuwania awamu ya tatu uongozini.

Hii leo habari kutoka Burundi zinasema kuwa mtu mmoja amepigwa risasi na kuuawa katika mji mkuu wa Bujumbura.

Image caption Rais Nkurunziza alikuwa akicheza dhidi ya marafiki zake

Mtu huyo alikuwa miongoni mwa waandamanaji wanaopinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa awamu ya tatu.

Walioshuhudia wanasema kuwa polisi walimpiga mwandamanaji huyo risasi mgongoni wakiwa katika eneo la Musaga linalotazamwa kama ngome ya upinzani.

Image caption Mechi hiyo ilikuwa mjini Bujumbura

Waandamanaji walijaribu kufika katikati mwa jiji la Bujumbura lakini walitimuliwa kwa mabomu ya moshi wa kutoa machozi.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewaomba zaidi ya raia laki moja na hamsini waliokimbia ghasia nchini humo katika majuma kadhaa yaliyopita, warejee nyumbani.

Image caption Rais Nkurunziza anatimu yake ''Hallelujah FC ''

Katika hotuba kwenye runinga ya taifa, amesema kuwa asilimia tisini na tisa nukta tisa ya Burundi ina amani.

Anasema kuwa hakuna mtu yeyote anayetaka kufufua taharuki ya kikabila.