Islamic State 'yadhibiti' Palmyra, Syria

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mji wa kale wa Palmyra umelipuliwa kwa silaha nzito nzito

Wanamgambo wa Islamic State wamechukuwa udhibiti wa karibu mji wote wa Palmyra, ulio na kivutuo kikubwa zaidi cha mahame ya kale.

Kuna hofu kwamba wanamgambo hao huenda wakaharibu mahame hayo ambayo shirika la Umoja wa mataifa kuhusu elimu, sayansi na utamaduni, Unesco, limetenga kama eneo la Urathi wa Dunia.

Vikosi vya serikali vimejiondoa katika mji huo baada ya wanamgambo hao kujongea, mmoja wa mashuhuda ameiambia BBC.

Wanamgambo wa IS wamebomoa maeneo kadhaa ya kali ambayo yalitangulia uwepo wa dini ya Kiislamu nchini Iraq ikiwemo miji ya kale ya Hatra na Nimrud.

Awali wanaharakati walisema kundi hilo linadhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa Tadmur, ambao ni mji wa kisasa ulio mkabala na Palmyra, baada ya kuwashinda wanamgambo walio watiifu kwa rais Bashar al-Assad.

'Makabiliano makali zaidi'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vita vya mji Palmyra

Televisheni inayomilikiwa na serikali nchini Syria imeripoti kuwa raia wameondolewa kutoka katika mji huo katika vurugu kali.

Omar Hamza, mwanaharakati katika mji wa Palmyra, ameiambia BBC kwamba eneo hilo ''limelipuliwa kwa silaha nzito'' na wanamgambo wa IS pamoja na serikali.

"kumekuwa na makabiliano pamoja na vurugu mbaya zaidi mashariki mwa mji huo," Bwana Hamza amesema.

"Vifaa vingi vya kihistoria vimehifadhiwa kusini mwa mji huo.

Vipo katikati ya mji huo na shamba linaloshikiliwa na wanamgambo wa IS, ambao wamelipua eneo hilo bila nia yoyote ya kuvilinda."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vifaa vingi vya kihistoria vimehifadhiwa kusini mwa mji huo.

Mamia ya sanamu za mji wa Palmyra zimeondolewa na kupelekwa eneo salama lakini minara mikubwa iliyopo maeneo ya kale zaidi ya mji huo haikuweza kuondolewa.

"Hili ni pambano la dunia nzima ," amesema mkuu wa turathi za kitaifa nchini Syria Maamoun Abdul Karim.

Ametoa wito kwa vikosi vinavyoongozwa na Marekani kuipinga Islamic State kuzuia wanamgambo hao ili wasiharibu eneo hilo.