CAF: Uchaguzi wa FIFA uendelee mbele

Image caption CAF yaunga mkono uchaguzi wa FIFA

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limendekeza uchaguzi wa urais wa shirikisho la soka duniani FIFA uendelee mbele kama ulivyopangwa.

CAF imesema kuwa hakuna sababu madhubuti ya kutosa kuhairisha uchaguzi mkuu.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya shirikisho, CAF imekariri kumuunga mkono rais Sepp Blatter licha ya shinikizo kutoka wadau la kumtaka ajiondoe madarakani kufuatia kukithiri kwa ufisadi ndani ya shirikisho analoliongoza

Blatter anawania muhula wake wa tano kama rais wa FIFA dhidi ya mwanamfalme Ali bin al-Hussein kutoka jordan .

"CAF inapinga jitihada zozote za kuhairisha uchaguzi wa urais ulioratibiwa kufanyika Mei tarehe 29''taarifa hiyo ilisema.

Aidha taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa Shirikisho hilo la Afrika litashirikiana kwa njia yeyote na uchunguzi dhidi ya shirikisho la soka duniani FIFA.

Image caption CAF imekariri kuwa itamuunga mkono Blatter

''CAF inaunga mkono jitihada za kuleta uwajibikaji miongoni mwa maafisa wanaosimamia soka katika FIFA.

Kama shirikisho la soka duniani ''Tunakataa kabisa ufisadi ndani ya michezo, na hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kulitia doa jina la shirikisho letu''

Awali shirikisho la soka barani Ulaya UEFA liliunga mkono pendekezo la kuhairisha uchaguzi mkuu.