IS yadaiwa kuuwa watu 20 Palmyra

Haki miliki ya picha AFP
Image caption IS yadaiwa kuuwa watu 20 Palmyra

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Syria, wanasema kuwa wanamgambo wa Islamic State, wametumia ukumbi wa zamani wa utawala wa Kirumi katika mji wa kale wa Palmyra, kutekeleza mauwaji ya wafungwa 20.

Shirika moja la Uingereza linalohudumu nchini Syria, linasema kuwa raia wa eneo hilo walikusanywa na Wapiganaji wa IS katika eneo wazi na kushuhudia namna wanavyowauwa watu hao waliokamatwa kwa kupigwa risasi.

Inakisiwa kuwa zaidi ya watu 240 wengi wao askari, wanawake na watoto wanadaiwa wameuwawa katika eneo hilo la Palmyra, tangu wanamgambo hao wa Islamic State walipouteka mji huo na eneo la kihistoria juma lililopita.

Awali mji huo ulikuwa ukidhibitiwa na serikali pamoja na makundi yanayoungwa mkono na serikali.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Watu 240 wengi wao askari, wanawake na watoto wanadaiwa wameuwawa katika eneo hilo la Palmyra

Kulikuwa na hofu kuwa wapiganaji hao wa Islamic State wataharibu mabaki ya mji huo kama ilivyokuwa huko Iraq katika mji wa Nimrud lakini picha za mji huo zinaonesha kuwa bado mabaki ya mji huo wa kale yamesimama wima.

Tangu juma lililopita wapiganaji hao wameteka kiwanja cha ndege pamoja na jela moja iliyoko karibu.