Benki kuu Nigeria yakumbwa na ufisadi

Haki miliki ya picha none
Image caption kashfa ya fedha nigeria

Wakuu katika shrika la kupambana na rushwa nchini Nigeria wanasema maafisa kadhaa kutoka benki kuu ya nchi hiyo wamepelekwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi wa kiasi kikubwa cha fedha za thamani ya mamilioni ya dola.

Pia baadhi ya maafisa wa benki za kibiashara wamo kwenye orodha hiyo ya watuhumiwa baada ya kushukiwa kuhusika kwenye udanganyifu mkubwa wa pesa.

Shirika hilo la kupambana na ufisadi The Economic and Financial Crimes Commission lilimeuelezea udanganyifu huo wa fedha kuwa walijaribu kuingiza katika soko la fedha noti ambazo zilikuwa tayari zimeondolewa kutoka soko hilo na zilitakiwa kuharibiwa kabisa kwa kuwa zimezeeka au kwa sababu nyengine yeyote.

Katika ulaghai huo wahusika wanasemekana walitengeneza vipande vya magazeti kwa kiwango na ukubwa sawa na hizo noti za kuharibiwa na kudanganya kuwa wanachoma noti hizo zilizopigwa marufuku na badala yake kuzirudisha kwa matumizi ya kila siku ya kifedha hivyo kujipatia faida kubwa ya fedha halisi.

Waliokamatwa ni maafisa 6 wa benki kuu ya Nigeria wanaofanya kazi mjini Ibadan na wafanyikazi 16 kutoka benki za kibinafsi ambao pia wanatuhumiwa kushiriki kashfa hiyo.

Haki miliki ya picha efcc website
Image caption Nigeria

Ufisadi na Udanganyifu huo umeipa hasara Nigeria ya zaidi ya dolla million 30.

Ingawaje kamata kamata hiyo ilifanyika kabla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari, wengi wanamuona kama ndiye kichochezi kikubwa kilichosababisha hatua hiyo kutokana na msimamo wake mkali wa kupambana na rushwa nchini humo.

Kwa miaka mingi vita dhidi ya ufisadi nchini humo vimewalenga zaidi walarushwa wadogo huku wala rushwa wakubwa wakikwepa mkono wa kisheria kwa kutumia hizo hizo fedha walizozipata kwa njia za kifisadi.