Nusu fainali za michuano ya French Open

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Andy Murray mcheza tenis wa Uingereza akitinga nusu fainali za michuano ya French Open ya mwaka 2015

Andy Murray amefanikiwa kumbwaga mpinzani wake David Ferrer kwa mara ya kwanza katika uwanja wa udongo na kutinga kwa mara ya tatu katika nusu fainali za French Open.

Mwingereza huyo wa tatu kwa ubora duniani kwa wanaume alishinda 7-6 (7-4) 6-2 5-7 6-1 na atakabiliana na Novak Djokovic anayeongoza kwa ubora katika mchezo huo wa tenisi kwa wanaume.

Ushindi huo unampeleka Murray katika hatua ya nusu fainali ya michuano mikubwa kwa mara ya 16.

Naye Rafael Nadal amesema atapigana kuhakikisha anarejea katika ubingwa wa michuano ya French Open baada ya kutolewa na Novak Djokovic katika hatua ya robo fainali. Hii ni mara ya pili kwa Nadal kufungwa mjini Paris.

Djokovic kutinga hatua ya nusu fainali amemshinda Nadal kwa seti 7-5 6-3 6-1 na sasa ana kwa ana na Andy Murray katika nusu fainali.

Na kwa upande wa kina dada, mchezaji nambari moja Serena Williams alihitaji dakika 65 tu kumrarua mpinzani wake Sara Errani kwa seti 6-1 6-3 na kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya French Open katika uwanja wa Roland Garros. Sasa atapambana na Mswiss Timea Bacsinszky. Huku bingwa mtetezi wa michuano hiyo kwa wanawake Maria Sharapova, ameng'olewa katika michuano hiyo kwa kucharazwa na Lucie Safarova kutoka Czech kwa seti 7-6 (7-3) 6-4.