Marekani inaamini itafanikiwa dhidi ya IS

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mapambano dhidi ya Islamic State yakiendelea

Ikulu ya Marekani imesema ina imani kwamba mkakati wa kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Iraq na kuwaorodhesha wapiganaji wa Kikabila wa Sunni utafanikiwa katika mapambano dhidi ya Islamic State.

Kauli hiyo imetolewa baada ya rais Barak Obama wa Marekani kupitisha mpango wa kupelekwa vikosi vya ziada vya wanajeshi mia nne na hamsini katika jimbo la Anbar ambapo wapiganaji wa IS wanashikilia eneo kubwa.

Vikosi vya Marekani vitafungua kituo cha tano cha mafunzo kitakachosaidia jeshi la Iraq kuwashirikisha makabila ya kisunni katika mapambano hayo- kigezo ambacho kinaonekana ni muhimu katika kuwatimua IS katika maeneo yanayokaliwa na idadi kubwa ya wasunni huko magharibi mwa Iraq.

"kwa kweli tunaendelea kuwa na imani kwamba jitihada za kuvijengea uwezo vikosi vya usalama vya Iraq, kuorodhesha wapiganaji wa makabila ya kisunni kwa kuwaleta pamoja chini ya amri ya udhibiti wa serikali kuu ya Iraq, itakuwa ni mkakati madhubuti dhidi ya ISIL mjini Anbar.

Katika kipindi cha muda mrefu, tunachotaka kufanya ni kujenga uwezo wa vikosi vya ndani na mamlaka za ndani kutawala haya maeneo na tumeona kwamba hiki ni kitu ambacho wamarekani na jeshi la marekani haliwezi kufanya kwa niaba ya Iraq, hiki ni kitu ambacho wairaqi sharti wakifanye wenyewe na tunataka kuwasaidia kuwajengea uwezo wa kufanya hivyo.