Walimu 126 wapigwa marufuku Kenya

Image caption BBC

Tume ya kuwaajiri walimu nchini Kenya TSC imewapiga marufuku zaidi ya walimu 100 ambao wamepatikana na hatia ya makosa kadhaa ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia.

Walimu hao sasa wameondolewa katika orodha ya sajili ya walimu na hawataruhusiwa kutoa hudumu yao katika shule yoyote nchini.

Katika ilani rasmi iliochapishwa katika Gazeti rasmi la serikali,tume hiyo imetoa orodha ya walimu 116 ambao wameachishwa kazi kwa kile tume hiyo inasema ni ukosefu wa nidhamu.

Taarifa hiyo inasema kuwa walimu hao waliachishwa kazi baada ya kuchukuliwa hatua za nidhamu ambazo ziliwapata na hatia ya makosa kadhaa.

Wawili kati ya wale waliopigwa marufuku ni wanawake.

Taarifa hiyo inaendelea kuonya kwamba mwalimu yeyote aliyepigwa marufuku na ambaye atapatikana akitoa huduma ya mafunzo nchini atapigwa faini isiozidi elfu tano ama kifungo cha miezi sita.

Walimu kadhaa wamepelekwa mahakamani huku wengine wakisimamishwa kazi baada ya kupatikana na hatia ya kuwabughudhi kingono wanafunzi.

Mwaka uliopita mwalimu wa shule ya upili katika mkoa wa magharibi alipelekwa mahakamani na kushtakiwa na kosa la kumlawiti mwanafunzi wa miaka 19.

Mwalimu mwengine ambaye alituhumiwa kwa kum'baka mwanafunzi wake alishtakiwa na baadaye kuhamishwa,hatua iliozua hisia kali huku wazazi na wanaharakati wa maswala ya kibinaadamu wakitaka mwalimu huyo kufungwa jela.

Afisa wa shirika linaloangazia maswala ya watoto nchini Kenya ambaye hakutaka kujulikana amemtaka mkurugenzi wa mashtaka ya uma kuchukua kesi hiyo ili kuhakikisha kuwa wale waliopatikana na hatia dhidi ya watoto wanafungwa.

Amesema kuwa walimu waliofutwa kazi ni tishio kwa watoto nchini Kenya.