Mpatanishi wa mzozo wa Burundi ajiondoa

Image caption Maandamano Burundi

Umoja wa mataifa umesema mjumbe wake maalum katika eneo la maziwa makuu hataendelea tena kuwa mpatanishi katika mzozo wa Burundi.

Msemaji wa umoja huo Vladimir Monteiro amesema mjumbe huyo Said Djinnit amejiondoa kutoka kwa harakati hiyo iliyokuwa inatafuta mwafaka kati ya vyama vya upinzani na kile kinachotawala cha rais Pierre Nkurunziza anayekabiliwa na shinikizo za maandamano kila uchao kupinga hatua yake ya kuwania muhula mwengine kama rais wa nchi hiyo.

Hakuna sababu zozote zilizotolewa kuhusu kujiondoa kwa bwana Djinnit lakini awali makundi ya upinzani yalikuwa yamedai kuwa afisa huyo alikuwa anaupendelea upande wa serikali madai anayoyakana.

Licha ya hatua hiyo bwana Djinnit ataendelea kuwa mjumbe maalum wa umoja wa mataifa katika nchi za maziwa makuu.