Wapenzi wakongwe zaidi duniani waoana

Image caption Wapenzi wakongwe zaidi duniani wafunga ndoa nchini Uingereza

Mwanaume mmoja Muingereza mwenye umri wa miaka 103 ameingia katika daftari za historia kwa kuwa bwana harusi mkongwe zaidi duniani.

Bwana George Kirby,alimpiga pambaja bi harusi, Doreen Luckie, mwenye umri wa miaka 92 na kula kiapo cha kuwa muaminifu kwake hadi kifo kitakapo watenganisha!

Bwana Kirby alisema kuwa bi Luckie humfanya akajisikia barubaru.

Aidha aliwavunja mbavu waliohudhuria sherehe hiyo aliposema kuwa wakati mwengine umri humlemea.

''niliogopa kupiga goti na kumuomba akubali kuwa kipenzi changu kwa raha na karaha kwa sababu nilihofia nikipiga goti nitashindwa kuinuka ''alisema Kirby.

Kirby na sabuni yake ya roho wamekuwa pamoja kwa takriban miaka 27 sasa kabla hawajaamua kufunga pingu za maiasha akisema kuwa ''anaona umri unasonga''.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bwana Kirby alisema kuwa bi Luckie humfanya akajisikia barubaru.

Bi harusi alivalia gauni leupe lenye maua ya samawati huku Kirby ambaye alikuwa ni bondia shupavu katika ujana wake akivalia suti japo aliletwa madhabahuni akiwa kwenye kiti chenye magurudumu.

Kwa pamoja wawili hao wamevunja rekodi ya dunia ya kuwa maharusi wakongwe zaidi.

Kwa jumla wanaumri wa miaka 195 ambayo ni miaka 7 zaidi ya rekodi ya awali ya maharusi wakongwe.

Rekodi ya awali ilikuwa ikishikiliwa na wapenzi wawili raia wa Ufaransa, Francois Fernandez na Madeleine Francineau.