Watu na Wanyama pori wasombwa Georgia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hata magari ya huduma ya dharura hayakusazwa

Mafuriko makubwa yaliyoikumba mji mkuu wa Georgia, Tbilisi,yamesababisha maafa makubwa huku watu 8 wakithibitishwa kufariki.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mafuriko yalitokana na mto Vere kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa

Lakini hiyo sio chanzo cha taharuki mjini humo.

Taharuki mjini humo inasababishwa na wanyama pori.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kiboko alipatikana katikati ya mji

Yamkini wenyeji wa mji huo wameombwa kukaaa majumbani mwao baada ya wanyama waliohifadhiwa katika hifadhi moja katikati ya mji huo kusombwa na mafuriko.

Wanyama waliotoweka ni pamoja na simba marara simba wa mwituni,dubu na hata mbweha.

Kati ya wale waliouawa watatu walipatikana ndani ya hifadhi hiyo ya wanyama.

Haki miliki ya picha n
Image caption Wanyama walitapakaa kote mjini wakitoroka mafuriko katika hifadhi yao

Kiboko mmoja alipatikana akihangaika mjini na akatekwa baada ya kudungwa sindano yenye madawa ya kumlewesha.

Makundi ya waokoaji yameanza kutembea nyumba hadi nyengine wakitafuta kuwaokoa manusura na kutathmini hasara iliyotokea baada ya mvua kubwa kunyesha.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Shughuli ya kuwarejesha wanyama katika hifadhi zimeanza

Watu kadha wamewachwa bila makao baada ya mvua kubwa kusababisha mto Vere kuvunja kingo zake.

Meya wa mji huo Davit Narmania amesema hali ni mbaya mno huku akiwaasa wenyeji wakae majumbani mwao ilikuzuia matukio ya uvamivizi wa wanyama pori.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanyama wengine hawakusazwa na mafuriko hayo

Wanyama kadha wamepatikana wakiwa wamekufa japo haijabainika wanyama wangapi bado wako hai.

Shughuli ya uokoaji inaendeshwa na makundi yanayopaa kwa helikopta na magari ya huduma ya kwanza.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Afisa katika afisi ya meya wa mji huo anakadiria hasara iliyotokea kuwa ni ya kima cha dola milioni kumi

Afisa mmoja katika jiji la Tbilisi anakadiria hasara hiyo kuwa huenda imefikia dola milioni kumi.

Hii si mara ya kwanza kwa mafuriko kusababisha maafa mjini Tbilisi, mwaka wa 2012 watu watano walipoteza maisha yao baada ya mto huo kuvunja kingo zake.