Gavana wa Benki kuu ya Kenya ''Hajaoa''

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wabunge nchini Kenya wazua kihoja baada ya Gavana mteule wa benki kuu ya Kenya kukiri kuwa hajao licha ya kuwa na umri wa miaka 54

Gavana mteule wa benki kuu ya Kenya Daktari Patrick Ngugi Njoroge amezua mjadala nchini Kenya baada yake kukiri kuwa hajaoa licha ya kuwa na umri mkubwa.

Daktari Ngugi Njoroge mwenye umri wa Miaka 54 aliteuliwa na rais Kenyatta kuwa gavana wa 9 katika benki hiyo baada ya kuibuka wa kwanza katika shughuli ya uteuzi iliyojumuisha wagombea 22 iliyofanyika majuzi.

Image caption Gavana mteule wa Benki kuu ya Kenya Patrick Ngugi Njoroge

Daktari Njoroge aliyasema hayo mbele ya kamati maalum ya wabunge waliokuwa wanamhoji kuambatana na Katiba ya Kenya.

Jopo hilo la wabunge hata hivyo lilipoteza mwelekeo na kufuatilia swala ibuka la yeye kuwa na umri wa miaka 54 na ''mwenye mshahara mkubwa'' ilihali hana jiko.

''Itawezekanaje kuwa unadonge nono na kazi nzuri na huna mke''

''Je unaweza kulinda pesa za wakenya na huna familia '' aliuliza mwanakamati mmoja.

Image caption Tangazao hilo la Gavana mpya limewasisimua wanawake ambao hawajaolewa kumuomba awaoe kupitia mtandao wa Twitter.

Daktari Njoroge anapokea mshahara wa shilingi milioni tatu za Kenya sawa na dola elfu 31 kwa mwezi.

''Je unafwata maadili ya jamii?'' Aliuliza mwanakamati mwengine.

Dakta Njoroge aliwajibu kwa kinywa kipana kuwa ''ni chaguo langu mimi kuwa pekee yangu.''

''Ninataka kuwahakikishia kuwa sijakiuka maadili ya jamii kwa njia yeyote ile, kwa hakika hamna hila kuhusu swala hili.''alisema gavana huyo mpya.

Wabunge hao mara walibadili mkondo tena na kumuuliza iwapo amewekeza katika sekta yeyote nchini Kenya.

Image caption Wakenya wengine wamemtania na kumlinganisha na Rais Obama

Dakta Njoroge alikanusha kuwekeza katika uchumi wa taifa lakini alikariri kuwa ameweka akiba ya pesa zake katika mabenki kadha nchini Kenya.

''Nafahamu kuwa sijawekeza katika uchumi wa taifa letu kwa sasa lakini siamini hali itaendelea kuwa hivyo katika siku zijazo''alisema Dakta Njoroge.

''Mimi ni mwanauchumi hodari kwa hivyo matumizi ya fedha kwangu ni ya ubanifu mno.''

Dakta Njoroge anashahada ya uzamifu ya uchumi kutoka chuo kikuu cha Yale.

Image caption Gazeti kubwa nchini Kenya Nation iliwaponda wabunge waliokuwa wakimchunguza kwa kupotosha mada kuu ambayo ni uchumi wa taifa na kupiga msasa maswala ya kibinafsi

Gavana huyo mteule kwa sasa ni mshauri wa rais wa hazina ya fedha duniani IMF.

Jopo hilo lilitumia muda mchache kuangazia swala la mfumuko wa bei ya bidhaa na kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya.

Shilingi ya Kenya imeshuka kwa kiwango kikubwa na sasa dola moja ya Marekani inabadilishwa na shilingi 97.

''Ninafahamu kinachoendelea katika uchumi wa Kenya lakini nikitulia nitarekebisha mara moja vipengee muhimu zitakazoboresha ushindani wa mabenki madogomadogo na pia kupunguza kiwango cha riba nchini Kenya.'' alisema dakta Njoroge.

Atachukua pahala pa Profesa Njuguna Ndun'gu aliyestaafu mwezi Machi.