Wanaharakati wa Ukimwi wampinga Kenyatta

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanaharakati wa Ukimwi wampinga Kenyatta

Wanaharakati wanaotetea watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi nchini Kenya wamewasilisha kesi mahakamani wakipinga agizo la rais Uhuru Kenyatta kutaka watoto wote wanaoishi na virusi hivyo kusajiliwa.

Wanaharakati hao wanamtaka rais afutilie mbali agizo hilo wakidai kuwa linakiuka haki za watoto hao na kusababisha unyanyapaa zaidi.

Mashirika mawili yasiyokuwa ya kiserikali, pamoja na walalamishi wengine wawili wa kibinafsi wamewasilisha kwa pamoja kesi hiyo mahakamani, sio kupinga azma ya rais Kenyatta kuwasaidia hususan watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi, bali kama wanavyodai wenyewe, ni kupinga mbinu inayotumiwa kuwasajili watoto hao.

Kwa mujibu wa Rais Kenyatta, anataka majina hayo yatolewe kwa serikali yake ili aweze kuunda mikakati muafaka ya kutoa huduma ya afya kwa watoto hao.

Mashirika hayo hata hivyo yanadai kuwa japo ni kweli kuna maelfu ya watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi wanaohitaji huduma hizi muhimu, kuwasajili kando kutahatarisha

vita dhidi ya unyanyapaa vilivyopiganiwa kwa miaka mingi.

Image caption Wanaharakati hao wanasema kuwa amri hiyo inakiuka haki zao za kikatiba

Pia wanasema ni ukiukaji wa haki zao za kikatiba.

Katika malalamiko yao kwa mahakama, watetezi hao pia wamezitaka wizara husika kulazimishwa kuficha majina hayo kwa kutumia kodi maalum au hata kuzifutilia mbali data zote walizokusanya kutokana na agizo hilo la rais.

Jaji wa mahakama ya juu nchini humo anayesikiliza kesi hiyo Mumbi Ngugi, ametoa ilani ya dharura kwa kesi hiyo na kuwaagiza wahusika wote kuwasilisha stakabadhi zote zinazohitajika kabla ya Jumatano, ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa.

Kwa mujibu wa Allan Maleche, mkurugenzi mkuu wa shirika la KELIN, mojawapo ya mashirika waliowasilisha kesi hiyo, usajili huo utakuwa na athari kubwa kuliko inavyokadiriwa sasa kwani itavunja msingi wa haki za kuwa a usiri wa kibinafsi hasa kwa watu wanaoishi na virusi hivyo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Kenyatta aliagiza kukusanywe data ya wagonjwa wa Ukimwi nchini Kenya

Agizo hilo la rais Kenyatta haliwagusi watoto peke yao, bali wanawake wote waja wazito walioambukizwa virusi hivyo pamoja na akina mama wanaonyonyesha watoto ambao pia wameambukizwa.

Katiba ya Kenya imeharamisha kunakiliwa, kurekodi au kuchapisha majina ya watu walioambukizwa virusi vya HIV ila kwa dharura chache ambapo pia imeelezwa kisheria chini ya kipengee kinacholinda haki za binadamu.

Mnamo Februari mwaka huu, Rais Kenyatta alitangaza agizo hilo akilenga kuunda miradi mahsusi itakayotoa huduma muafaka za afya kwa watoto wanaoishi na virusi hivyo nchini Kenya.

Watetezi wengi wa haki za binadamu hata hivyo wamepinga mfumo unaotumika kuwasajili watoto hao ambapo wanalazimishwa kuandikisha majina yao kamili, shule wanakosomea na hata jamaa wao wote walio na ushirika nao au kuathirika vyovyote na kuugua kwao.

Takwimu za maambukizi ya virusi vya HIV nchini Kenya zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni moja nukta sita wameambukizwa virusi vya hivyo hatari, takriban nusu milioni kati yao ni watoto.